Mahakama nchini Kenya imeamua kuwa ushuru wa nyumba uliozua utata ulioanzishwa na rais William Ruto haukuwa halali.
Ushuru wa asilimia 1.5 kutoka katika mishahara ya Wakenya wote wanaolipa ushuru, iliyohitaji waajiri watoe hivyo pia, ulitiwa saini kuwa sheria mwezi Juni ili kufadhili mpango wa nyumba za bei nafuu.
Ushuru huo ilikuwa kati ya mapendekezo ya mabadiliko katika sheria ya fedha ya nchi.
Kamati ya majaji watatu katika Mahakama Kuu jijini Nairobi ilisema Jumanne kuwa hakukuwa na mfumo kamili wa kisheria wa kuanzishwa kwa ushuru huo.
Pia wamesema kuwa kutengwa kwa wafanyakazi wasio rasmi kutokatwa kodi hiyo ilikuwa ni "ubaguzi na kutokuwa na mantiki,"
Amri ya kungoja
"Amri imetolewa kukataza kukusanywa kwa ushuru huo...unaojulikana ushuru wa nyumba za bei nafuu," alisema hakimu David Majanja.
Serikali imeomba mahakama itoe amri ya kusitisha uamuzi wake.
Ushuru huo uliwekwa kama sehemu ya sheria ya fedha ambayo ilipandisha ushuru kwa bidhaa mbalimbali katika hatua ambayo imekuwa na athari katika nchi ambayo tayari imeathiriwa na mfumuko wa bei.
Hasira juu ya kupanda kwa bei, hasaa kwa bidhaa za msingi kama vile chakula na mafuta, ilisababisha msururu wa maandamano dhidi ya serikali ya Ruto mapema mwaka huu.