Mahakama nchini Kenya imemsamehe Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya Gilbert Masengeli kwa kosa la kuidharau mahakama. Masengeli alikuwa amehukumia kifungo cha miezi sita Septemba 13, 2024.
Masengeli alifika mbele ya mahakama hiyo Ijumaa na kuiomba radhi mahakama kwa matukio yaliyotokea hadi yeye kuhukumiwa.
"Masengeli alihojiwa na mawakili na uchunguzi wangu ni kwamba majibu yake yalionekana kuwa ya kweli. Mahakama hii ina uhakika kwamba Masengeli anajuta," Jaji Larence Mugambi alisema leo katika uamuzi wake.
Masengeli alihukumiwa kifungo cha miezi sita na Jaji huyo baada ya kukosa kufika mahakamani moja kwa moja kutoa ufafanuzi kuhusu kupotea kwa watu watatu tangu Agosti 2024.
Masengeli alisimama mbele ya mahakama Ijumaa na kusema kuwa hakukusudia kufanya hivyo.
Alimwambia Jaji Lawrence Mugambi kwamba alihusika katika masuala ya usalama wa kitaifa ambayo yalihitaji umakini wake wa kipekee katika eneo la kaskazini mwa Kenya.
“Nakuheshimu wewe na mahakama zetu zote kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuzingatia utawala wa sheria, mimi nikiwa askari polisi ni wajibu wangu kusimamia amri za mahakama na kuhakikisha amri za mahakama zinafuatwa,” alisema Masengeli.
"Naomba mahakama hii ikubali msamaha wangu na iondoe hatia na hukumu."
Waliopotea wapatikana
Wanaharakati watatu wanaodaiwa kutekwa nyara Agosti 2024 kufuatia maandamano ya kuipinga serikali waliripotiwa kuachiliwa Ijumaa asubuhi.
Bob Njagi, Aslam Longton na kaka yake Jamil Longton waliachiliwa nje ya jiji la Nairobi siku ya Alhamisi, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu lilisema.
Wanaume hao wanadaiwa kutekwa na vikosi vya usalama kwa wiki kadhaa na mahakama ilikuwa inamtaka Masengeli kutoa maelezo ya kina.
Naibu Mkuu wa Polisi aliiambia mahakama kuwa juhudi zilifanywa kuhusiana na kutoweka kwa watatu hao ambao ni wakazi wa Kitengela jijini Nairobi na uchunguzi bado unaendelea.
Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha, watatu hao wamepatikana leo asubuhi.
Masengeli ameisisitizia mahakama kuwa watu hao watatu hawakuwa mikononi mwa polisi na kudai kuwa, leo asubuhi amepata taarifa za kupatikana kwao kupitia wakili wao Nelson Havi alipokuwa akiitarifu mahakama kuhusu kupatikana kwao.
“Mimi siko juu ya sheria, nimetii amri za mahakama,” alisema Masengeli wakati akitetea haki yake ya kuendelea kushika wadhifa wa umma.
Jaji ajiondoa kwa kesi
Baada ya kutengua hukumu yake dhidi ya mkuu huyo wa polisi jaji Mugambi alitangaza kuwa hatahusika tena na kesi hiyo.
"Ninafanya uamuzi wangu wa kujitoa katika kuendelea na kesi hii kwa sababu za kibinafsi," aliongezea.
Baada ya kuhukumiwa Septemba 16, 2024 Masengeli alikashifiwa na Jaji Mkuu wa Kenya kwa kuondoa walinzi wa Jaji Mugambi ambaye alimhukumu.
Hata hivyo, wakati huo Naibu huyo wa Polisi alijitetea kwa kusema kuwa wa mujibu wa sheria, Rais, Naibu Rais na Rais Mstaafu ndio pekee wanastahili kupata maafisa binafsi wa usalama.
Akidai kuwa alikuwa amewaondoa maaskari hao kwa ajili ya kwenda kupata mafunzo zaidi.