Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli. Picha na Huduma ya Taifa ya Polisi Kenya. 

Mahakama nchini Kenya imempata Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli na hatia ya kutoiheshimu makakama.

Hati hii imetokana baada ya Masengeli kukosa kufika mahakamani kwa mara ya sita, licha ya hakimu kusisistiza kuwa anahitajika.

"Ni jukumu la Mahakama kurejesha imani ya umma na mahakama. Inspekta jenerali anaweza kuondolewa ofisini ikithibitishwa kwamba anahujumu katiba," Jaji Lawrence Mugambi alisema.

Mugambi amesisitiza kuwa maafisa wa serikali katika ofisi za umma kama Kaimu IG lazima wafuate katiba.

Mahakama itatangaza hukumu yake dhidi ya Masengeli siku ya Ijumaa.

Wakili wa serikali aliyemuakilisha Masengeli aliiambia Mahakama siku ya Jumatatu kwamba Kaimu huyo yupo kazini katika eneo la Wajir.

Masengeli alitakiwa kuielezea mahakama kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa ndugu wawili na mwanaharakati, watatu hao wakiwa wametoweka kwa wiki mbili.

Kaimu IG alikuwa ameagizwa kufika mbele ya hakimu ana kwa ana kueleza ni kwa nini watu hao watatu waliotekwa nyara huko Kitengela, Nairobi hawajaachiliwa.

Ndugu wawili Jamil Longton, Aslam Longton, na mwanaharakati Brian Njagi inaripotiwa walichukuliwa na watu waliovalia suti waliodai kuwa ni maafisa wa polisi kutoka Nairobi lakini hawakutoa sababu ya kuwakamata.

Watatu hao inaripotiwa walitekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi mnamo Agosti 19, 2024.

Wakili wao Nelson Havi alihoji ni kwa muda gani mahakama itamruhusu kaimu IG kupuuza wito wa mahakama kwa mapenzi yake na hata kumtuma Naibu wake kumuwakilisha.

Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo aliunga mkono maoni ya Havi.

"Kaimu IG alikuwa Pwani wiki iliyopita akipiga picha na kufanya mazungumzo na watu badala ya kutii amri ya mahakama," alisema.

TRT Afrika