Rais wa Senegal ametangaza muda wake wa urais utakwisha ifikapo Aprili 2 na majadiliano ya kupanga uchaguzi kwa ajili ya mrithi wake kuanza wiki ijayo.
Akizungumza katika mahojiano ya vyombo vya habari katika mji mkuu wa Dakar, Macky Sall amesema, tarehe ya kufanya uchaguzi aliousogeza mbele inabaki kuwa wazi, lakini anapanga kuachia nafasi yake kama rais baada ya mwisho wa kipindi chake.
"Aprili 2, 2024, kazi yangu inaisha kama rais wa Senegal," amesema.
"Kuhusiana na tarehe, tutaona kutokana na majadiliano, ambayo yanategemea kuanza Jumatatu, Februari 26 na pengine kuisha Jumanne. Makubaliano yasipofikiwa, kila kitu kitapelekwa katika Baraza la Katiba," amesema.
" Uchaguzi unaweza kufanywa kabla ya Aprili 2," ameongeza.
Sall ametangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais wa Februari 25, akitaja kuwepo kwa mgogoro wa orodha wa wagombea urais and madai ya kuwepo kwa ufisadi miongoni mwa majaji wa katiba.
Baadae Bunge la Taifa lilipitisha mswada wa kuahirisha kura mpaka Disemba 15 huku vikosi vya ulinzi vikivamia jengo na kuwatoa wabunge wa upinzani.
Lakini Baraza la Katika la Senegal lilitangaza uamuzi wa kusogeza mbele uchaguzi kuwa ni kinyume cha katiba na kubatiliza uamuzi huo.
Ucheleweshaji wa uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Magharibi umeibua vurugu na maandamano, ambapo watu watatu waliuawa na wengine kukamatwa.
Waandamanaji wanamtuhumu Sall kwa kutumia sababu zisizo na msingi kuahirisha uchaguzi, muda mfupi kabla ya kampeni kuanza.