Vikosi vya usalama vya Senegal vimetawanya umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika mji mkuu wa Dakar siku ya Jumapili kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais wa Februari 25.
Rais Macky Sall alitangaza Jumamosi kuwa kura hiyo itacheleweshwa hadi tarehe ambayo haijatajwa kutokana na mzozo kuhusu orodha ya wagombea - hatua iliyokataliwa na vyama vya upinzani.
Takriban waandamanaji 200 walizuia msongamano wa magari kwenye barabara kuu mjini Dakar kwa kizuizi cha muda cha matairi yaliyokuwa yakiungua, shirika la habari la Reuters linaripoti.
Waziri mkuu wa zamani 'akamatwa'
Waziri mkuu wa zamani wa Senegal Aminata Toure, ambaye sasa ni kiongozi mkuu wa upinzani, alikamatwa kwenye maandamano ya kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais, mbunge wa upinzani Guy Marius Sagna aliambia AFP.
"Ninathibitisha kuwa Aminata Toure amekamatwa na askari," alisema. Toure aliteuliwa kuwa waziri mkuu na Rais Macky Sall kabla ya kujiunga na upinzani.
Umati wa wafuasi wa upinzani walioandamana walijificha kwenye barabara za kando baada ya polisi wa kutuliza ghasia kurusha vitoa machozi. Mamlaka bado haijatoa maoni juu ya matukio ya hivi karibuni.
Senegal haijawahi kuchelewesha kura ya urais na hakuna uhakika kuhusu nini kitatokea baadaye.
ECOWAS inahimiza utulivu
Mwaka jana, nchi hiyo ilikumbwa na maandamano mabaya baada ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kufungwa jela, huku wafuasi wake wakisema ni njama ya kumzuia asigombee katika uchaguzi huo.
Kwa miongo kadhaa, Senegal inaonekana kama mojawapo ya nchi zenye demokrasia imara katika Afrika Magharibi lakini matukio ya hivi majuzi ya kisiasa nchini humo yamezua wasiwasi.
Baada ya tangazo la Sall kupitia televisheni, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ilionyesha wasiwasi wake kuhusu mazingira yaliyosababisha kuahirishwa na kutaka tarehe mpya ya uchaguzi kupangwa haraka. Pia ilitoa wito kwa utulivu na mazungumzo.