Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amemtaka waziri mkuu wake kuandaa "mpango wa utekelezaji" wa dharura wa kuimarisha uchumi na fedha wenye kupiga hatua nchini humo, ofisi yake ilisema katika taarifa yake.
Kiongozi huyo mwenye miaka 44 alipata ushindi katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita kwa ahadi ya mageuzi makubwa, na kuwa rais mwenye umri mdogo zaidi licha ya kuwa hajawahi kushika wadhifa huo.
Siku ya Jumanne alimpa waziri mkuu na mshauri wake wa zamani Ousmane Sonko hadi mwisho wa mwezi kuandaa "mpango wa utekelezaji", ilisema taarifa hiyo, iliyotolewa baada ya mkutano wa kwanza wa baraza la mawaziri la Faye.
Alimuamuru Sonko "kufanyia mapitio ya jumla ya programu na mipango" na kutoa taarifa kuhusu "hali ya jumla ya fedha za umma", ushirikiano wa kimataifa na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, ilisema.
Makataa ya mwisho wa mwezi
Aliielekeza serikali kukamilisha mpango huo ifikapo mwisho wa mwezi na kutekeleza "bila kuchelewa, na sekta ya binafsi ya nchi hiyo na kuhuisha upya uchumi wa taifa".
Aliwaambia mawaziri kuwa amechaguliwa ili kuhakikisha kunakuwepo na "mabadiliko katika viwango vyote vya maisha ya kiuchumi na kijamii" nchini humo.
Mtu mmoja kati ya watatu nchini Senegal anaishi katika dimbwi la umaskini huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikifikia asilimia 20.
Mfumuko mkubwa
Uchumi wa nchi hiyo ulikabiliwa na changamoto ya janga la Uviko na athari za vita vya Ukraine.
Madeni na mfumuko wa bei vinazidi kuongezeka huku miaka mitatu iliyopita ya mivutano ya kijamii na kisiasa ikizuia uwekezaji.
Akizindua baraza lake la mawaziri siku ya Ijumaa, Sonko alisema vipaumbele vya serikali vitajumuisha ajira kwa vijana, kupunguza gharama ya maisha na kulinda haki za binadamu.