Tangu mwaka 2001 baada ya bunge la taifa kuidhinisha , kila mwaka tarehe 9 mwezi Juni, Uganda imetenga tarehe 9 Juni , kwa ajili ya kumbukumbu ya wale waliopoteza maisha katika vita vya ukombozi kati ya mwaka 1981 - 1986.
Vita hivi maarufu kama vita vya Luwero, ilikuwa mapigano kati ya tawi rasmi la serikali ya Uganda la Jeshi la Ukombozi wa Kitaifa (U.N.L.A.) na vikundi kadhaa vya waasi, lakini haswa waasi wa National Resistance Army (N.R.A.).
Inakadiriwa kuwa karibu kati ya watu 100,000 hadi 500,000, ambao ni pamoja na wapiganaji na kiraia, walikufa katika sehemu tofauti nchini.
Rais Yoweri Museveni ameongoza Uganda tangu mwaka 1986.
"Tuwakumbuka wanaume na wanawake mashujaa ambao waliweka taifa mbele katika kutafuta uhuru wa nchi yetu," ikulu ya taifa ya Uganda imesema katika mtandao wake wa twitter.
Vita hivyo viliharibu vijiji kadhaa na kuharibu maisha ya watu vibaya sana hivi kwamba serikali ya sasa bado inafanya kazi ya kujenga upya miundombinu iliyoangushwa na uchumi.
Je, kwa miaka 41 Uganda imefanya maendeleo gani ?
Uganda imeweka sekta tofauti kama vipengele muhimu vya maendeleo huku ikijitadihi kujikwamua kiuchumi licha ya changamoto ya kindani na kimataifa.
Kilimo kimewekwa kama sekta muhimu zaidi ya uzalishaji kiuchumi. Bishara nje ya nchi pia imenawiri, kutokana kwa mauzo ya chakula .
Takwimu za kutoka kwenye hotuba ya rais Yoweri museveni zaonyesha katika mwaka 2022, nchi ilikuwa imeuza magunia milioni 5.7 ya kahawa yenye thamani ya dola za milioni 858.7 kwa nchi za nje.
Mauzo mengine nje ya nchi ambayo yamefanya vizuri ni pamoja na samaki kwa thamani ya dola za Marekani milioni 166, maharage yenye thamani ya dola za Marekani milioni 132, sukari (Dola 146 milioni), mahindi (dola za Marekani milioni 131) na bidhaa za viwandani zenye thamani ya US$348.9m.
Utalii nchini ni mojawapo ya chanzo cha mapato makuu, ikiwa kwa sasa sekta hiyo inaajiri moja kwa moja jumla ya watu milioni 1.55 nchini Uganda na huchangia 6.7% ya pato la taifa la nchi.
Uganda imejitahidi katika viwanda kwa ajili ya jujenga uwekezaji wa ndani wa bidhaa.
Uganda sasa ina maeneo nane ya viwanda katika sehemu tofauti nchini, huku tatu zikifanya kazi chini ya ushirikiano wa kibinafsi na umma. Jumla ya viwanda ni 4008, na imetoa ajira kwa watu150,000.
Katika elimu serikali inawekeza katika kutoa elimu kwa viwango vyote kwa wananchi ikiweka msisitizo kwa elimu ya ujuzi , ili iwape hasa vijana uwezo wa kujiajiri.
Serikali inasema itafanya kazi katika kuongeza mapato ya ndani na pia kuhakikisha gharama zinapunguzwa.
Ndio maana iliamua kuboresha idara za serikali na kufikisha huduma kwa kila mtu hadi kijijini ili kuhakikisha pesa za walipa kodi zinawarudia kama huduma bora .
Serikali inasema changamoto bado ipo katika kuboresha uzalishaji wa bidhaa, kuweka huduma za afya kila mahali nchini na kuboresha miundombinu ya usafiri.
Uganda iligundua ina rasilimali ya mafuta zaidi ya miaka 20 iliyopita. Ina akiba ya ghafi ya mapipa bilioni 6.5, lakini hadi sasa haijaanza kuzalisha kibiashara .
Inaangalia sekta hii kama mojawapo ya chanzo cha mapato makubwa ambayo yatabadilisha kabisa hali ya uchumi ya wananchi wake kuwa bora zaidi.
Lengo la Uganda ni kuanza uzalishaji mwaka 2025.