Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC) imesikitishwa na uamuzi wa kampuni ya madawa ya Moderna kubatilisha mipango yake ya awali ya kujenga kiwanda cha uzalishaji wa chanjo barani.
Moderna, Inc. ni kampuni ya dawa na teknolojia ya kibayoteknolojia yenye makao makuu Marekani.
" Ingawa tunakubali kwamba mahitaji ya chanjo ya Uviko-19 yamepungua kwa kiasi kikubwa, barani Afrika na ulimwenguni kote, ni muhimu tutafakari juu ya uamuzi wao," Africa CDC ilisema katika taarifa.
Tarehe 7 Machi, kampuni ya Moderna ilitangaza mpango wake kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo barani Afrika. Mchakato huo ulilenga kuwekeza dola milioni 500 kuzalisha hadi dozi milioni 500 ya chanjo kila mwaka kwa ajili ya bara la Afrika.
Ilipofika Machi 20, 2023, kampuni ya Moderna ilitangaza kuwa imefikia makubaliano na serikali ya Kenya ili kuanzishwa kwa kiwanda cha uzalishaji wa chanjo nchini Kenya. Kiwanda hicho kingekuwa ni cha mfano kwa bara la Afrika.
Lakini sasa kampuni hiyo imebadili mipango hii. Kampuni ya Moderna ilisema katika taarifa kuwa imesitisha mipango yake ya kujenga kiwanda cha kuzalisha chanjo nchini Kenya.
" Moderna imesitisha juhudi zake za kujenga kituo cha utengenezaji wa mRNA (chanjo) nchini Kenya huku ikibainisha mahitaji ya baadaye ya chanjo za mRNA katika bara la Afrika. Mahitaji barani Afrika ya chanjo za COVID-19 yamepungua tangu janga hili na haitoshi kusaidia uwezekano wa kiwanda kilichopangwa nchini Kenya," Moderna ilisema.
" Moderna haijapokea maagizo yoyote ya chanjo kwa Afrika tangu 2022 na imekabiliwa na kufutwa kwa maagizo ya hapo awali, na kusababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 1," iliongezea.
Afrika ilikumbwa na janga la Uviko-19 mwaka 2019, huku ikikumbana na changamoto za upatikanaji wa chanjo ya maradhi hayo kutokana uzalishaji mdogo wa nchi zilizoendelea.
Umoja wa Afrika, AU, ulianzisha hazina ya AU ya kukabiliana na Uviko-19 na kuzindua Mfuko wa Upataji Chanjo wa Afrika (AVAT) kwa usaidizi wa benki ya Afrexim.
AVAT iliweza kupata chanjo milioni 400 kutoka kwa wazalishaji wengine isipokuwa Moderna, kwa sababu chanjo za Moderna hazikupatikana, licha ya majaribio ya kununua.
Africa CDC inasema kuwa asilimia chini ya 5 ya chanjo za Uviko-19 barani Afrika, zilitoka Moderna.
" Licha ya juhudi hizi za Kiafrika, chanjo ya Uviko-19 bado iliwasilishwa kwa kuchelewa kwa Afrika, muda mrefu baada ya chanjo kupatikana kwa nchi zilizoendelea," Africa CDC imesema.
Umoja wa Afrika umesema Moderan haifai kualumu Afrika kwa ukosefu wa mahitaji ya chanjo ya Uviko-19 ikidai kwa Moderna kusimamisha mipango ya kutengeneza chanjo barani Afrika, inatumika tu kuendeleza ukosefu wa usawa ambao ulionekana duniani wakati wa Uviko-19.
" Kulaumu Afrika na Afrika CDC kwa ukosefu ilhali watengenezaji wengine wa chanjo wanaendelea na mipango na ujenzi wao barani Afrika, Moderna inaachana na dhamira ya kujenga uwezo unaohitajika na unaofaa wa utengenezaji wa chanjo barani Afrika," Africa CDC imesema.
Uzalishaji wa chanjo Afrika
Kampuni ya Ujerumani ya BioNTech tayari imefanya makubaliano na Rwanda kuweka kiwanda cha kuzalisha chanjo. Mipango ya ujenzi ilianza rasmi Desemba 2023.
Kampuni hiyo imesema Inapanga kukamilisha majengo yote katika eneo la Kigali na kuanza mafunzo ya ndani ya wafanyikazi maalum katika kituo hicho mnamo 2024, na uzalishaji wa chanjo na tayari kwa uthibitishaji mnamo 2025.
Kampuni hiyo imewekeza jumla ya takriban dola milioni 150 ili kukamilisha ujenzi wa eneo hilo ikijumuisha vitengo vya utengenezaji.
Umoja wa Afrika inasema kuwa kwa sasa, mahitaji ya chanjo barani Afrika yanathaminiwa kuwa zaidi ya dola za Marekani bilioni 1 kila mwaka, na takwimu hii inakadiriwa kukua pamoja na idadi ya watu barani humo katika miongo kadhaa ijayo.
Afrika tayari inachangia karibu asilimia 20 ya idadi ya watu duniani, lakini sekta ya chanjo ya bara hutoa tu karibu aslimia 0.2 ya usambazaji wa kimataifa.