Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Baada ya jitihada za kukita mizizi kwenye nchi zinazozungumza Kiingereza, Kifaransa na Kireno kufanikiwa, sasa ni zamu ya nchi zinazozungumza lugha ya Kispanyola.
"Kongamano hili linafanyika nchini Cuba ili kulenga nchi zinazozungumza lugha ya Kispanyola, huku tukijenga ushawishi kwenye nchi hizo baada ya kufanya hivyo kwenye nchi zinazozungumza Kiingereza, Kifaransa na Kireno," Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA), Consolata Mushi anaiambia TRT Afrika
Kulingana na Mushi, maandalizi ya kongamano hilo yamefikia asilimia 90 huku Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuhudhuria tukio hilo.
Pamoja na mambo mengine, tukio hilo litashuhudia uzinduzi wa Kamusi ya Kihispania kwenda lugha ya Kiswahili, ambayo imeandaliwa na Chuo Kikuu cha Havana na kijitabu kidogo chenye misemo ya kila siku ya Kispanyola kwenda Kiswahili ambacho kimeandaliwa na BAKITA.
"Kumekuwepo na mkataba wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Chuo Kikuu cha Havana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku kukiwa na maprofesa wanne waliosoma Dar es Salaam kwenye miaka ya 70," anaeleza Katibu Mtendaji huyo wa BAKITA.
Mbali na vitabu hivyo, kongamano hilo litanakshiwa na onesho la kanga pamoja na 'usiku maalumu wa mswahili', ambao utatawaliwa na vyakula na urithi wa utamaduni wa mswahili.
"Kutakuwa na maonesho ya kazi za sanaa na utamaduni ambayo yataambatana na usiku wa Mswahili, ngoma za asili, muziki wa Kitanzania, masimulizi ya uhusiano ambao umedumu kwa miaka mingi kati ya watu wa Cuba na Tanzania na maonesho ya kanga," anasema Mushi katika mahojiano maalumu na TRT Afrika.
Kwanini Cuba?
Mushi anasema uamuzi wa kuandaa kongamano hilo la kimataifa nchini Cuba, unatokana na historia nzuri ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, kama ulivyoasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Fidel Castro wa Cuba.
Na kwa sababu hiyo, tayari sehemu mojawapo ya uwanja wa mashujaa wa Afrika nchini Cuba, imetengwa maalumu kwa ajili ya sanamu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
"HivI tunavyozungumza, mtoto wa Mwalimu Nyerere aitwaye Madaraka Nyerere tayari ameshawasili kushuhudia tukio hilo kubwa na la heshima kwa nchi yetu," anasema.
Mbali na sanamu ya Mwalimu Nyerere, eneo hilo pia limewekwa sanamu za viongozi mbalimbali wa Afrika wakiwemo Jomo Kenyatta wa Kenya na Laurent-Désiré Kabila kutoka DRC.
Kama ishara ya kuthamini mchango wa Cuba kwenye kukuza lugha ya Kiswahili kwenye ulimwengu wa Kihispania, Tanzania imeandaa zawadi mbalimbali kwa wenyeji wao, ikiwemo 'kinyago cha ujamaa', chenye kuwakilisha uhusiano wa kijamaa baina ya nchi hizo, mlango wa Zanzibar na picha ya Mlima Kilimanjaro.
Mwamko wa Kiswahili ukoje nchini Cuba?
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa BAKITA, kumekuwepo na mwamko mkubwa wa kujifunza lugha ya Kiswahili nchini Cuba, hali inayoashiria dalili njema kwa siku zijazo.
Mushi anaamini kuwa, Cuba itakuwa ni kichocheo cha kukuza lugha ya Kiswahili kwenye 'ulimwengu wa Kihispania'.
"Inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 600 watakuwepo kushuhudia kongamano hili la kimataifa na hii inatupa sababu na imani kubwa juu ya kusambaa na kutandaa kwa lugha ya Kiswahili kwenye ulimwengu huu," anabainisha.
Mtendaji huyo wa BAKITA anaamini kuwa nafasi ya lugha ya Kiswahili inabakia kuwa kubwa duniani, huku mashirika mbalimbali ya kikanda na kimataifa yakiendelea kuitambua lugha hiyo.
Mkutano Mkuu wa UNESCO uliofanyika Novemba 23, 2021 uliamua kuwa, siku ya Kiswahili Duniani iadhimishwe kila mwaka.
Kwa sasa, Kiswahili ni lugha ya taifa kwa nchi kadhaa ikiwemo Tanzania, Uganda na Kenya.
Lugha nyingine zinazotambulika duniani ni kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kirusi, Kispanyola na Kiarabu.