Tanzania yasaini mikataba ya bandari ya Dar es Salaam na DP WORLD

Tanzania yasaini mikataba ya bandari ya Dar es Salaam na DP WORLD

Soma zaidi ndani uelewe mabadiliko yaliyofanyiwa vipengee vilivyoleta utata katika mkataba huu
  Serikali inauwezo wa kuvunja mkataba muda wowote, kwa kuweka wazi sababu za kutoridhishwa / Picha TRT Afrika 

Na Idd Uwesu

TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania

Tanzania imesaini mikataba mitatu kwa ajili ya uwekezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es salaam, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino huko Dodoma.

Mikataba hiyo iliyotiwa saini kupitia usimamizi wa bandari Tanzania TPA na DP World inahusisha upangishaji na uendeshaji wa Gati namba 4 hadi 7 za bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa Mikataba hiyo, Rais wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa hatua hii inafikiwa baada ya kufanya uchambuzi wa kina ikiwemo maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Watanzania wa kada mbalimbali

“Serikali kwa upande wake ilisikiliza michango na maoni mbalimbali yaliyotolewa na Chama cha wanasheria wa Tanganyika, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati huru na vyombo vya habari,'' alisema Rais Samia. ''Pia tuliangalia maoni katika mitandao ya kijamii. Tumewasikiliza viongozi wetu wa dini na baadhi ya viongozi wetu wastaafu” aliongeza Rais.

Aidha Rais Dr. Samia alisema uwekezaji unaokwenda kufanywa na kampuni ya DP World utakwenda kubadilisha utendaji wa bandari ya Dar es Salam na kuiwezesha kuchangia zaidi katika pato la Taifa.

“Tumesema kwamba kila pale ambapo sekta binafsi inaweza ikaweka fedha na serikali tukaweka fedha zetu kwenye mambo mengine ya maendeleo ya Jamii ni bora zaidi, tunawakaribisha wawekezaji zaidi waje wawekeze tufanye biashara wapate na sisi tupate ili mapato ya serikali tuyapeleke kwenye matumizi mengine.'' alisem Rais Samia.

Dondoo muhimu ndani ya mikataba hiyo

  • Mkataba utakuwa na muda wa ukomo usiozidi miaka 30

  • Watalipa kodi zote za Serikali kwa mujibu wa Sheria

  • Kutakuwa na utaratibu wa kukagua kazi na utekelezaji wa mkataba kila baada ya miaka mitano

  • Serikali itachukua 60% ya mapato au faida

  • Serikali inauwezo wa kuvunja mkataba muda wowote, kwa kuweka wazi sababu za kutoridhishwa

  • Mkataba huu sio wa gati zote za Bandari ya Dar es Salaam gati ambazo hazipo kwenye mkataba huu zinatafutiwa mwekezaji mwingine (mbali na DP World)

  • Mkataba huu hauhusishi Bandari yoyote ya mwambao wa Bahari ya Hindi wala maziwa makuu.

Mabadiliko katik amkataba yanasema DP WORLD  Watalipa kodi zote za Serikali kwa mujibu wa Sheria/ Picha :TRT AFRIKA

Akitoa maelezo ya Mikataba hiyo kabla ya utiaji saini, Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa alilaumu ukosefu wa miundombinu ya kisasa kusababisha kuzembea katika utenda kazi bandarini.

Ukusanyaji kodi wa TRA utaongezeka maradufu

Mbossa aliongeza kuwa serikali imekua ikitumia takriban 90 % ya mapato yote yanayokusanywa katika uendeshaji wa maeneo yaliyokodishwa na kubakia na10 % kama faida.

“Tumekuwa tukikusanya fedha na katika kila shilingi 100 tunayokusanya tunatumia shilingi 90 kugharamia huduma na kubakia na shilingi 10, hivyo Kutokana na mikataba hii serikali itaweza kubakia na zaidi ya asilimia 60 ya mapato yote ya maeneo ambayo tunayakodisha kwa sababu gharama zote za uendeshaji zitakua zinakwenda kwa kampuni ya DP World” alisema Mbossa.

“Mkataba huu ambao hauhusishi bandari zingine ikiwemo za maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa pia utakua ukipima utendaji wa kampuni ya DP World kwa kila miaka mitano,'' aliendelea kuelezea Mbossa.

Moja ya faida kubwa ya uwekezaji huo imeelezewa kuwa kuongezeka kwa makusanyo kodi, ushuru wa forodha na tozo mbalimbali ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA itaweza kukusanya shilingi za Tanzania Trilioni 26.7 kufikia mwaka 2032 tofauti na sasa ambapo Mamlaka hiyo inakusanya Shilingi Trilioni 7.8 kwa mwaka.

Nae Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya DP World, Sultan Ahmed Bin Sulayem alisema kuwa katika miaka mitao ya mwanzo DP World itawekeza Dola milioni 250 huku kazi ya kwanza ikiwa ni kuboresha miundombinu ya kushughulikia mizigo kwa haraka ili kuondoa kero ya ucheleweshaji wa mizigo unaoikabili Bandari ya Dar es Salaam hivi sasa.

“Tutaimarisha jukumu la bandari kama lango la bahari kwa ukanda wa shaba na maeneo mengine muhimu ya madini ya nishati ya kijani,'' Alisema Sultan. ''Tutafanya hivyo kwa mpango wa awamu nyingi ambao pia utalenga kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kupitia nje ya Tanzania na kuingia nchi kavu.” aliongezea Sultan.

Licha ya hatua hii, bado kunao Watanzania wengi wanaotilia shaka mikataba hii wakiona pengine kuna vipengee vilivyofichika ndani yake vitakavyokuja kuwaponza baadaye.

Hata hivyo serikali imejitokeza leo kubainisha mengi ya masuala yaliyokuwa na utata mwanzoni ikiwemo kubwa zaidi kuwekwa muda wa ukomo wa mkataba miongoni mwa mengine.

Mchumi na mhadhiri wa chuo kikuu cha Kimataifa cha Kampala tawi la Dar es Salaam Dr. Bravious Kahyoza aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa ipo hatari ya kubinafsisha viungo vikuu vy Uchumi kama Bandari kwa wawekezaji binafsi.

TRT Afrika