Kufungwa kwa kampuni za sukari katika mikoa ya Magharibi na Nyanza kutokana na uhaba wa miwa kumechangia kupanda kwa bei ya sukari nchini. / Picha: Reuters

Rais William Ruto amewaahidi wakulima kuwarudhishia thamani yao ya kukuza miwa.

"Tutahakikisha kampuni ya sukari ya Nzoia inarejea kazini ndani ya mwaka mmoja," rais William Ruto alisema.

Kampuni ya Nzoia ni mojawapo ya kampuni za sukari ambazo zimekwama kwa sababu tofauti ikiwemo uhaba wa miwa.

Kwa sasa kuna mvutano kati ya wawekezaji wakubwa wawili kuhusu nani ambaye anafanya kampuni kubwa ya sukari inayoitwa, Mumias Sugar kutofanya uzalishaji.

"Mambo ya ubinafsishaji, eti ndiyo shamba ya wananchi ipatiwe mtu mwingine tutasimamisha. Hayo mambo ya kuuza shamba ya wakulima tulisimamisha, tukafuta mpango wa ubinafsishaji," ameongezea.

Kufungwa kwa kampuni za sukari katika mikoa ya Magharibi na Nyanza kutokana na uhaba wa miwa kumechangia kupanda kwa bei ya sukari nchini.

Nchi inategemea asilimia 100 ya sukari kutoka nje ili kukidhi mahitaji yake ya sukari nyeupe iliyosafishwa.

Sukari kutoka nchi za nje zilifika hadi tani 426,334 mwaka 2021.

Mwezi Agosti mwaka huu serikali ilitangaza kuwa wasagaji wa sukari ya umma na binafsi hawatapewa idhini ya kuagiza sukari kutoka nje.

Katika miezi minne wafanyabiashara binafsi wataruhusiwa kuagiza sukari kutoka nchi za nje ya tani 100 na 200.

Hii ni kwa ajili ya serikali kujitahidi kupunguza bei ya sukari ambayo kwa sasa iko juu sana, kwa takribani dola 2 kwa kilo.

Nchi inategemea asili mia 100 ya sukari kutoka nje ili kukidhi mahitaji yake ya sukari nyeupe iliyosafishwa /Picha: Reuters 

Uingizwaji wa sukari haramu nchini na makampuni ya biashara pia umechangia kuzorota kwa sekta ya sukari.

Sekta ya Sukari ina changamoto gani?

Sekta ndogo ya sukari inasaidia zaidi ya Wakenya milioni nane ambao hupata riziki zao moja kwa moja kutoka kwa uzalishaji wa sukari na kwa njia moja au nyingine.

Lakini wizara ya kilimo inasema kuwa uzalishaji wa sukari ndani ya nchi unabadilika na unaendelea kushuka chini ya mahitaji licha ya uwezo.

Ripoti ya wizara ya kilimo inasema kuwa zaidi ya wakulima 300,000 husambaza miwa kwa wasagaji.

Kuna viwanda 16 vya sukari nchini vyenye uwezo wa kusindika jumla ya tani 51,450 za miwa kwa siku lakini uwezo wao kwa sasa ni karibu 56% tu.

Rais wa Kenya William Ruto amesema ataondoa hali ya kikundi kidogo tu cha wawekezaji kutawala sekta ya sukari/ Picha kutoka kwa rais William Ruto 

Wataalam wanasema sababu za uzalishaji wa chini ni pamoja na Upungufu wa matumizi unatokana na uhaba wa vifaa vya kiwandani matengenezo, usambazaji unaobadilika-badilika wa miwa na teknolojia isiyofaa ya usindikaji.

Pia kuna makampuni yanayotumia mashine za zamani.

Rais Ruto anasema kuwa mashirika ya kibiashara yamekatisha ajenda ya serikali ya kufufua makampuni ya seriklai ya sukari.

Kando na uagizaji rasmi wa sukari, Kenya kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliana na changamoto ya sukari isiyo ya hali bora inayoingia soko la ndani.

TRT Afrika