Jumanne, mfalme wa Uingereza Charles III, na mkewe Malkia Camilla walikaribishwa rasmi katika Ikulu ya Kenya na rais wa nchi hiyo William Ruto. Mapokezi hayo pia yaliambatana na salamu ya mizinga 21 ukiashiria heshima kwa kiongozi huyo.
Ziara hii inakuja huku kenya ikijitayarisha kusherehekea miaka 60 ya uhuru ifikapo Disemba, 12, ambapo Kenya ilipata Uhuru kutoka kwa Uingereza.
Chini ya utawala wa Uingereza tangu mwishoni mwa karne ya 19, Kenya ilikuwa rasmi koloni la Uingereza mnamo 1920.
Ziara ya Mfalme Charles III inajiri wakati ambapo nchi kadhaa zilizotawaliwa na Uingereza, zinaitaka nchi hiyo kukiri makosa ya unyanyasaji yaliyofanywa katika kipindi cha ukoloni.
Baadhi ya jamii kutoka kabila la Wakikuyu na Wakalenjini nchini Kenya wamemtaka Mfalme huyo kukiri makosa ambayo wakoloni waliifanyia jamii hizo huku wakitaka Uingereza kurudisha baadhi ya rasilimali zilizochukuliwa kutoka Kenya.
Ziara wa Mfalme inahusisha pia kukutana na baadhi ya vijana ambao wamewekeza ubunifu wao katika teknolojia.
Waheshimiwa hao, Rais Ruto na mkewe walitembelea eneo jijini Nairobi lenye mti unaoitwa Mũgumo katika bustani ya Uhuru Gardens Nairobi.
Mti huo unaashiria mahali ambapo, usiku wa Disemba 12, 1963, Kenya ilisherehekea uhuru wake kwa kushushwa bendera ya muungano na kupandishwa kwa bendera ya Kenya.
Wakati wa uasi wa Mau Mau wa 1952-1960 katikati mwa Kenya, Wakenya 90,000 waliuawa au kulemazwa na 160,000 kuzuiliwa, Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) imekadiria.
Serikali ya Uingereza hapo awali ilielezea masikitiko yake kwa unyanyasaji huo na ilikubali kulipa fidia ya malipo ya pauni milioni 20 ($ 24 milioni) mnamo 2013.
Mfalme wa Nandi Koitalel Arap Samoei aliongoza uasi wa miaka kumi hadi alipouawa na kanali wa Uingereza mwaka wa 1905. Katika miaka iliyofuata, Waingereza walichukua sehemu kubwa ya ardhi na ng'ombe za watu wake.