Na Charles Mgbolu
Mwimbaji maarufu wa Uganda Ssemanda Manisul, anayejulikana kitaalamu kama King Saha, alikuwa jukwaani akitumbuiza usiku wa kuamkia leo wakati maafisa wa polisi walipovamia ukumbi huo na kumwamuru asimamishe onyesho na kushuka jukwaani.
Ilizua ghasia kubwa katika ukumbi huo na kwenye mitandao ya kijamii, huku uvumi ukienea mara moja kwamba Saha amepelekwa “mahali pasipojulikana.”
King Saha hatimaye alikuja kwenye mitandao ya kijamii ili kuondoa hofu, lakini kisha akawashutumu polisi kwa unyanyasaji.
“Polisi wa Uganda mkiwa na kesi dhidi yangu niiteni; usije ukavuruga shoo yangu. Mnawatia hofu mashabiki wangu,” Saha aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram muda mfupi baada ya tukio hilo.
Historia ndefu na polisi
Hii si mara ya kwanza kwa mwanamuziki huyo wa Biri Biri, ambaye ni mshindi wa tuzo kadhaa, zikiwemo Tuzo za Uganda Entertainment (UEA), HiPipo, na Rising Star Award katika anga ya muziki wa Uganda, kumenyana na polisi.
Mnamo Mei, alipigwa marufuku na mamlaka kutumbuiza katika sherehe ya kifahari ya ufunguzi wa Uwanja wa Nakivubo wenye viti 35,000.
Polisi wa Uganda wamejibu hasira za kijana huyo mwenye umri wa miaka 34 kwenye mtandao wa kijamii.
Luke Owoyesigire, Naibu Msemaji wa Polisi wa Metropolitan ya Kampala, aliambia vyombo vya habari kuwa hali kwenye hafla hio ilikuwa "ya machafuko" wakati Saha alipopanda jukwaani.
"Kulikuwa na watu wengi, hapakuwa na nafasi yoyote ya kuegesha magari, na nafasi ilikuwa ndogo sana," Owoyesigire alisema.
'Hatari kwa watu'
Polisi pia waliwaamuru wamiliki wa biashara hiyo kufunga biashara usiku huo kwa sababu ukumbi huo ulikuwa na "idadi kubwa ya watu."
"Onyesho lenyewe lilionekana kama tamasha, na watu wa usalama walikuwa na wasiwasi kwa sababu hatukufahamishwa kamwe kuihusu. Hakukuwa na ukaguzi ufaao kwenye mlango, tulidhani hii inaweza kuhatarisha watu".
Baadhi ya Waganda kwenye mitandao ya kijamii, hata hivyo, wana wasiwasi kwamba polisi wanazidi kupunguza maonyesho ya kisanii ya wanamuziki nchini humo.
Tayari kuna marufuku ya matamasha ya muziki yenye sauti kubwa na matukio yanayopita saa nne jioni bila vibali.
'Kutofanyika tena'
Wasanii wengine wameikemea mamlaka kwenye mitandao ya kijamii kwa kile ambacho wengine wamekielezea kama ukandamizaji wa ubunifu.
Lakini mamlaka zinasisitiza kuwa tukio hili la hivi punde linahusu kuzuia janga la kutisha kutokea tena.
Takriban watu tisa, wakiwemo watoto watano, walifariki katika msongamano wa watu wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa 2023 katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Tukio hilo lilitokea katika kituo cha biashara ambacho kilikuwa na maonyesho ya fataki, huku umati mkubwa wa watu ukitokea baada ya watu waliotoka kuona fataki hizo kulazimika kurudi kwenye ukumbi huo.