Mwezi wa Juni kila mwaka unashuhudia kusomwa kwa bajeti za nchi kadhaa za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na Kevin Momanyi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mwezi Juni kila mwaka unashuhudia kusomwa kwa bajeti kuu za nchi kadhaa za Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani EAC kwa ajili ya mwaka mpya wa fedha.

Lakini utamaduni huu wa nchi kusoma bajeti kwa wakati mmoja ulianzia wapi na kwa nini?

Rwanda, Uganda, Kenya, na Tanzania zimekuwa zikifanya hivi kulingana na maelekezo ya mwaka 2010 ya Baraza la Mawaziri la EAC.

Wanafanya hivyo ili kuoainisha sera zao za kifedha ili kuendana na matakwa ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na hatimaye Sarafu moja.

Sababu nyengine ni kuepusha uwezekano wa nchi moja kujinufaisha kwa kushusha au kupandisha kodi kwa faida yake dhidi ya nchi nyingine.

Kwa mfano, Kenya ingesoma bajeti yake na kupanga bei ya mkate kuwa shilingi 60, Tanzania ingefuata mfano huo wiki au miezi kadhaa baadaye na kuweka bei yake kuwa shilingi 50 na wiki chache baadaye Rwanda pengine ingefuata mkondo huo na kupanga bei ya mkate huo huo kuwa shillingi 45 halafu Uganda nayo ikaweka shillingi 40.

Hii itakua na athari katika soko la kanda la Afrika mashariki.

Mwaka huu ni Tanzania, Kenya, Uganda na Sudan Kusini zitakazosoma bajeti zao kwa wakati mmoja.

Hii ni kutokana na kwamba, Rwanda imeshasoma bajeti yake mwezi wa 5 mwaka huu kwa sababu inaelekea kufanya mchaguzi mkuu mwezi Julai, 2024.

Kwa upande mwengine, Somalia na DRC hazitosoma bajeti zao siku hiyo hiyo, kwani bado hazijaainisha sera zao za kifedha na jumuiya ya EAC. Hata hivyo, bajeti za mwaka huu wa fedha kutoka nchi za Afrika Mashariki, zimejikita katika vipao mbele kadhaa, ikiwemo miradi ya kimkakati pamoja na uwekezaji katika miundombinu muhimu.

Wakati huo huo, wananchi wanategea macho kuona ni kwa kiasi gani bajeti ya mwaka huu itaathiri maisha yao ya kila siku, hasa ikizingatiwa kwamba, kumekuwa na mapendekezo ya kuongeza kodi katika bidhaa muhimu kama vile mafuta ya kupikia.

TRT Afrika