Akihutubia taifa siku ya Ijumaa, Rais Ruto alisema tarehe ya kufunguliwa kwa shule itaahirishwa hadi pale tutakapotoa taarifa, akibainisha kuwa hali huenda kuwa mbaya zaidi siku zijazo.
Ruto pia aitoa wito kwa washirika wa kimaendeleo kusaidia kukabilaina na athari za tabianchi ili kupunguza mahangaiko ya wakazi.
Hapo awali shule zilipangwa kufunguliwa tena Aprili 29, 2024, lakini tarehe hiyo baadaye ilisukumwa hadi Mei 6, 2024, kutokana na kukatizwa na mvua kubwa.
"Hakuna kona ya nchi yetu iliyoepukana na maafa haya, tarehe ya kufunguliwa tena kwa shule zetu baada ya likizo ya Aprili iliyopangwa Jumatatu wiki hii, ilibidi ibadilishwe, usafiri umekuwa changamoto katika maeneo mengi ya nchi kutokana na mafuriko," Ruto alisema.
Aidha Ruto alisema hadi sasa watu 210 wamefariki kutokana na mafuriko hayo, huku wengi wakijeruhiwa na mali ya thamani isiyojulikana kuharibiwa.
Maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya udongo katika kaunti mbalimbali pia yametambuliwa kuwa maeneo hatarishi ambapo wakaazi katika makazi hayo wataanza kuhamishwa.