Kevin Mwachiro sasa ana nafuu baada ya miaka 10 ya matibabu dhidi ya saratani ya 'Mutliple Myeloma' . Picha:

Na Dayo Yussuf

Saratani huwapa watu mitihani kwa njia ambazo hakuna mtu anayeweza kujiandaa. Nguvu, imani, uthabiti, nia na huruma vinatiliwa shaka mwili unapotatizika na akili ikiyumba.

Mkenya Kevin Mwachiro amepitia haya yote na mengine. "Itakuwa miaka tisa Oktoba hii," anasema siku ambayo aligunduliwa kuwa na Saratanni aina ya Multiple Myeloma.

Siku ya kawaida mjini nairobi, siku iliyowaka jua vyema ilimhimiza yeye kutoka nje kwa ajili ya kukimbia katika bustani moja ya umma karibu na nyumbani kwake.

Maumivu makali ya ghafla kwenye mgongo wake yalimsababisha kuanguka. Kama alivyokuja kugundua katika siku chache zilizofuata, ulikuwa mwanzo tu wa safari ya masaibu ya yasiyofikirika.

"Nilikimbizwa hospitalini kwa gari la wagonjwa. Kwa kifupi, madaktari walijaribu vipimo vingi na kisha kuniambia nilikuwa na Multiple Myeloma," Kevin, ambaye sasa yuko katika hali ya remission ( yaani seli za saratani zimedhibitiwa) , anaiambia TRT Afrika.

Katika Multiple Myeloma, seli za plasma za saratani hujilimbikiza kwenye uboho, ambayop ni kipande laini ndani ya mifupa yetu ambapo seli za damu huundwa.

Seli za saratani geni hufurika kwa haraka seli za damu zenye afya. Badala ya kutengeneza kingamwili zinazosaidia, seli za saratani huzalisha protini zinazoathiri mwili wa mtu.

Multiple myeloma hutokea  wakati seli za plasma za saratani zinapo zaana kwenye uboho. Pich a: Getty

Kevin alikuwa na uelewa mdogo wa ugonjwa huo wakati huo. Isitoshe, mbali na hofu ya kupambana na adui asiyeonekana mwilini mwake, alijua kwamba matibabu ya saratani yangekuwa ya muda mrefu, na ya gharama kubwa.

Akili juu ya mengine yote

Ingawa miji kama Nairobi sasa ina vifaa vya hali ya juu vya matibabu ya saratani na matunzo mazuri, bado ni gharama kubwa kwa wengi. Na hali kama hii inashuhudiwa pia kwa nchi nyingine nyingi za Kiafrika.

Wengi wa watu waliogunduliwa na ugonjwa huo hupoteza matumaini mwanzoni. Kuna chaguo la kusafiri nje ya nchi, haswa kwa nchi kama India ambazo zinatoa matibabu ya bei nafuu, lakini hata hilo ni jambo ambalo sio kila mtu anaweza kumudu.

Kama Kevin anavyoshuhudia, kutoa ushauri kwa wagonjwa na familia zao ili kuepuka hofu ni ufunguo wa ufanisi wa udhibiti wa saratani. "Saratani haimaanishi hukumu ya kifo, na hilo ni jambo ambalo watu wanahitaji kuambiwa," anaelezea.

"Ikiwa watu wanaamini kuwa uwezekano wako wa kuishi ni mkubwa zaidi ikiwa utagunduliwa mapema, hawataona saratani kama hukumu ya kifo."

Kevin pia anaamini kuwa bila kujali ubora wa matibabu, huenda isifanye kazi ikiwa akili haiko tayari kuondoa wasiwasi .

Kevin Mwachiro ni mhanga wa saratani na anasema si hukumu ya kifo tena. Picha: Kevin Mwachiro

"Nilikuwa na shangazi ambaye tulimzika mwezi huo huo kabla ya utambuzi wangu, na nilijiambia, 'Sifi moyo. Hii haitakuwa hadithi yangu.' Nilijiingiza katika hali ya kujizatiti kuishi baada ya il ehofu ya mwanzo. Hilo lilinisaidia sana," anaiambia TRT Afrika.

Visa vinaongezeka

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya saratani barani Afrika imekuwa ikiongezeka kwa njia ya kutisha.

Mnamo 2020, takriban visa vipya vya saratani milioni 1.1 viligunduliwa katika bara hilo. Takriban vifo 700,000 viliripotiwa.

Takriban nusu ya wagonjwa wapya barani Afrika ni saratani ya matiti, shingo ya kizazi, tezi dume, saratani ya utumbo mpana na ini.

Habari njema ni kwamba huduma ya afya imepiga hatua za haraka katika kukabiliana na ongezeko la saratani, ikiwa ni pamoja na kuzuia.

"Tunapongeza hatua iliyofikiwa katika kuzuia na kutibu saratani katika eneo letu. Kwa mfano, nchi 17 barani humo zimeanzisha uchunguzi wa hali ya juu kulingana na mapendekezo ya WHO," Dk. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, anasema.

Lakini bila kujali maendeleo haya, kupata watu kutii itifaki za kinga na utunzaji mahususi za saratani ni changamoto.

Kulingana na wataalamu, jumuiya nyingi za Kiafrika zinachelewa kuzingatia ratiba za chanjo na kushiriki katika majaribio, jambo ambalo linarudisha nyuma miaka ya nyuma ya utafiti.

Kevin anasema msisitizo unafaa kuwa katika kuhakikisha watu wanasikia ujumbe - kwamba utafiti wa kisayansi umeendelea kwa kasi na mafanikio ni makubwa, na saratani kadhaa sasa zinaweza kuzuilika.

"Kwa sasa, tuna chanjo ya HPV ya saratani ya shingo ya kizazi, lakini upokeaji wake ni wa chini sana. Kila msichana nchini Kenya anapaswa kuwa kwenye chanjo hiyo...kila msichana," anasema.

Mazingatio kwa wauguzaji na watunzaji

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa matibabu ya saratani hayahusishi madaktari, wauguzi na wagonjwa pekee.

WHO inazitaka serikali kuweka kipaumbele katika kutunza na kuzuia saratani. Picha : Taasisi ya Kitaifa ya Saratani ya Kenya

Kevin anakubali kwamba ni muhimu kujenga mfumo sahihi wa usaidizi. "Nadhani hatuthamini vya kutosha walezi na wengine wanaotuona katika safari, haswa siku ngumu zaidi," anasema.

"Jizungushie watu ambao watakupa motisha na sio kukukatisha tamaa. Watafute marafiki wanao kushangili ana kukutia moyo. Hakuna nafasi kamwe ya kujitilia shaka au kuwa na fikira mbaya," anashauri wanaopitia mtihani wa matibabu ya saratani.

Kati ya 2022 na 2024, mada ya Siku ya Saratani Duniani mnamo Februari 4 ilikuwa "Funga pengo la saratani". Kampeni hiyo ilifungwa kwa kiapo cha kushinikiza serikali kuweka kipaumbele katika utunzaji wa saratani. Kwa mujibu wa WHO, kaulimbiu hiyo inahusisha mahitaji ya kimataifa ya nchi kuwekeza zaidi katika kuzuia na kutunza saratani.

Na kwa kutia hamasa, kuna hadithi ya Kevin - na ile ya mamilioni ya wengine kote ulimwenguni ambao wamepigana na kushinda dhidi ya saratani.

TRT Afrika