Wizara ya afya ya Uganda imetoa idhini kwa maabara mbili pekee kufanya uchunguzi wa DNA kujua baba wa mtoto.
Maabara ya Government Analytical na MBN Clinical zilizochaguliwa ziko katikati ya mji mkuu Kampala.
"Hakuna maabara na zahanati zitaruhusiwa kukusanya sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa DNA ya baba isipokuwa ziwe na makubaliano na maabara hizi mbili," waziri wa afya wa Uganda Dr. Jane Ruth Aceng ameambia waandishi wa habari.
Bunge lililalamika kuwa wanaume wengi wamepigwa na butwaa kwa kukuta wanalea watoto wasio wao baada ya kufanyia uchunguzi wa DNA.
Idara ya uhamiaji inasema wanaume 32 wameomba pasipoti za watoto wao zisimamishwe baada ya kupata wao sio baba zao.
Waziri amesema makubaliano hayo yatahusisha maabara hizi zingine kupeleka sampuli kwa zile mbili zilizochaguliwa kwa ajili ya uchunguzi. Ni hizo mbili tu zitawajibika kutoa matokeo.
"Maabara yoyote ambayo imetayarishwa na inataka kufanya uchunguzi wa DNA ya baba inaweza kutuma maombi kwa mkurugenzi mkuu wa huduma za afya ambaye ataunda timu ya wataalam kuangalia kama maabara iko sawa."
Wizara hiyo imesema hakuna maabara au kituo chochote kitakachosafirisha sampuli zozote za upimaji wa DNA nje ya nchi isipokuwa kwa kibali maalum kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa Huduma za afya na au Baraza la Kitaifa la Sayansi na Teknolojia la Uganda.