Na Charles Mbhoglu
Takriban kilomita 1,000 kutoka pwani ya Petite Côte ya Senegal katika Magharibi mwa Afrika kuna kisiwa kisichoishiwa watu, chenye mandhari nzuri ya milima ya volkano, fukwe za kuvutia, na wanyama pori wa kipekee lakini lenye ardhi kavu na jangwa lisilo na shughuli za kibinadamu.
Mpaka miaka ya 1990, kisiwa cha Santa Luzia huko Cabo Verde au Cape Verde kilikuwa na watu wanaoishi na walikuwa wanatumia kisiwa hicho kuwalisha mifugo. Lakini ukame wa ardhi uliwafanya watu wengi zaidi waondoke.
Kisiwa cha Santa Luzia ni sehemu ya funguvisiwa la Cabo Verde, kilichoko kati ya visiwa vya São Nicolau na São Vicente - karibu na pwani ya Magharibi mwa Afrika.
Cabo Verde inajumuisha visiwa kumi vya volkano na eneo la ardhi la takriban kilomita za mraba 4,000.
Santa Luzia ni kisiwa pekee kisichoishiwa watu katika mzunguko wa visiwa. Ni mahali lenye kuvutia sana, lakini watalii wachache jasiri wanathubutu kulitembelea.
Maji meupe safi na uzuri wa ufukwe na juu angani kuna milima mirefu iliyopasuka ya rangi ya kijivu inayotoweka kwenye ukungu uliong'aa.
Kisiwa hicho kinatanuka takriban kilomita 34.2 na hubadilisha muonekano wake kama kinyonga - kubadilisha mandhari yake ili kuzoea mazingira yasiyotabirika: yenye kijani na yenye rutuba wakati wa mvua mnamo Septemba, lakini kavu na gubikwa na ukame kwa sehemu kubwa ya mwaka ambapo kawaida hakuna mvua.
Kivutio cha Watalii
Santiago, Fogo, Maio, Brava, Boa Vista, Sal, São Vicente, Santo Antão, na São Nicolau ni visiwa vingine tisa vyenye jumla ya idadi ya watu karibu 600,000 kufikia mwaka 2021, kulingana na takwimu za sensa rasmi.
Mwezi wa Januari pekee, Cabo Verde ilipokea zaidi ya wageni 300,000 wakifurika kwenye visiwa hivyo tisa. Licha ya athari za Uviko-19, Cape Verde ilizalisha karibu dola milioni 169.00 mwaka 2020 kutoka sekta ya utalii, kwa mujibu wa World Data Info.
Biosfera ni kikundi cha watu wa hiari kinachofanya kazi ya kusafisha kisiwa hicho na kuwahudumia spishi mbalimbali za wanyama.
"Santa Luzia ina mfumo wa ikolojia dhaifu ambao unahitaji kulindwa. Ingawa hakuna watu wanaoishi hapa, tuna watu wa hiari ambao wanafanya kazi katika hali ngumu bila maji safi, bila mfumo wa kupoza na wamekatwa kabisa mawasiliano," anasema Biosfera kwenye tovuti yao.
Walakini, wavuvi kutoka visiwa jirani vya São Vicente na Santo Antão huvua samaki katika maji yanayozunguka kisiwa hicho kisichoishiwa watu.
Kihalali, Santa Luzia sio sehemu ya manispaa yoyote. Lakini inadhibitiwa na serikali kuu ya Cape Verde.
Mwaka 1990, visiwa vya Santa Luzia, Ilhéu Branco, na Ilhéu Raso vilipewa hadhi ya kuwa maeneo yaliyohifadhiwa. Santa Luzia iko kwenye orodha ya awali ya Maeneo ya Urithi wa Dunia ya UNESCO.