Na Coletta Wanjohi
Ushelisheli, nchi yenye visiwa 115 katika Bahari ya Hindi, nje ya Afrika Mashariki, imekua kivutio kikubwa cha watalii duniani, lakini wakaazi wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa visiwa vyao kuzama.
James Pierre mvuvi katika ufuo wa Beau Vallon, katika kisiwa cha Mahe anasema wameshuhudia bahari ikiendelea kusogea nchi kavu, na akiba ya samaki inapungua.
“Tulizaliwa kando ya bahari, tumeishi kando ya bahari, tunajua kila kitu kuhusu bahari," anaiambia TRT Afrika, na kuongeza, "Zamani kulikuwa na samaki wengi, sasa wanapungua, samaki wanatoweka, siku hizi kuna kiwango kidogo sana cha samaki majini tukilinganisha na zamani."
Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni yaani World Meteorological Organization, linaonya kwamba kiwango cha bahari kinaendelea kuongezeka.
Wanasayansi nao wanasema kwamba ongezeko hilo husababishwa na maji yanayotokana na barafu kuyeyuka na maji ya bahari yanapopata joto na kupanuka.
Athari hii ya mabadiliko ya tabianchi yanaonekana katika mataifa mengine ya visiwa vidogo katika kanda ya Afrika Mashariki kama vile Cape Verde, Mauritius, Réunion, Komori na Jamhuri ya Kidemokrasia ya São Tomé na Príncipe.
TRT Afrika ilizungumza na Dkt. Nirmal Shah, ambae ni Mkurugenzi Mkuu wa Shrika linalojishughulisha na Uhifadhi ya Mazingira yani Nature Seychelles, nae anasema mataifa ya visiwa vidogo yanalazimika kusogea mbali bahari.
"Tunaweza kuchukua baadhi ya miundombinu muhimu kutoka karibu na bahari na kwenda mahali pengine, lakini hiyo inahitaji kiasi kikubwa cha fedha," Dkt. Shah anaelezea. "Ni suala ambalo nadhani watu kutoka nchi kubwa hawaelewi kabisa na hawaelewi aina ya tishio linalotukabili,” anasema.
Suluhisho nyengine katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi (COP 27) uliofanyika nchini Misri mwaka jana, Muungano wa Mataifa ya Visiwa Vidogo ulipongeza kuundwa kwa hazina ya kukabiliana na hasara na uharibifu duniani.
Dkt. Shah, anaiambia TRT Afrika kwamba uamuzi huo ingawa ni muhimu kwa nchi za visiwa vidogo lakini haukutoa maelezo mwafaka kuhusu hazina hiyo na iwapo itatumika na nchi zilizoathirwa na mabadiliko ya tabianchi au la.
"Hatuna maelezo kuhusu suala zima la muundo wake, ni pesa ngapi zitaingia ndani yake,” anafafanua Dkt. Shah.
"Je itakuwa kama bima kama vile ya Umoja wa Ulaya au kama aina nyengine ya ufadhili kwa sekta kibinafsi na uwekezaji wa athari na kadhalika ambayo ni ngumu sana kwa nchi za visiwa vidogo?" Anauliza.
Anatahadharisha kuwa ni muhimu kwa watu kuelewa kuwa hata kuwepo kwa hazina hii kuna masuala ambayo hayawezi kurekebishwa.
"Hili ni jambo ambalo nadhani watu hawaelewi kabisa, kwamba tunaweza jaribu kurekebisha vitu fulani kama miamba ya matumbawe, lakini hatuwezi kurekebisha uharibifu uliofanyika ambao ni wa milele,” amesema Dkt. Shah.
“Tunapoteza ardhi, na maeneo ya pwani milele. Hatuwezi kuzirudisha. Tunapoteza riziki za watu na huo ndio mwisho wake kwa sababu uwanda mzima ambapo watu hupanda mboga, matunda umejaa chumvi, hivyo ni vigumu sana kukarabati hilo.”
Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wakaazi kama vile James, wanaonekana kupoteza matumaini,
“Hapana, hakuna suluhu, hakuna ufuo uliobaki. Suluhisho ni kuiacha kama ilivyo,” anasema.
Kwa upande wake, wataalamu wa mazingira kama Dkt. Shah wanaamini kuwa suluhisho la kudumu litatokea ikiwa nchi zote duniani zitaweka juhudi zaidi kupunguza hewa chafu duniani na kupunguza viwango vya joto.