Mkuu wa baraza la mpito la Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan anatarajiwa kukutana na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir mjini Juba.
Kulingana na Shirika la habari la kitaifa la Sudan, SUNA, Abdel Fattah Al-Burhan, amefunga safari mapema leo kuelekea mjini Juba, Jamhuri ya Sudan Kusini, kwa ziara rasmi.
Katika ziara hiyo Al Burhan ameandamana na Makamu wa Rais wa Baraza la Mpito la Utawala, Bwana Malik Aqar Air, Waziri wa Mambo ya Nje Sudan, Balozi Ali Al-Sadiq, na Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi Luteni Jenerali Ahmed Ibrahim Mufaddal.
Katika ziara yake, Mkuu huyo wa Baraza tawala la Sudan na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Salva Kiir Mayardit, ili kujadili mwenendo wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Aidha, mazungumzo kati ya viongozi hao yatagusia namna ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, masuala ya maslahi ya pamoja, ikiwemo maendeleo ya nchi hizo mbili na hali nchini Sudan.
Miongoni mwa viongozi wengine watakaoshiriki kwenye mazungumzo baina ya nchi hizo mbili ni pamoja na Luteni Jenerali Muhammad Al-Ghali Ali Youssef, Katibu Mkuu wa Baraza la Utawala, na baadhi ya mawaziri. .