Paul Mackenzie , kiongozi wa imani ya njaa ameshitakiwa leo katika Mahakama Kuu ya Malindi, nchini Kenya.
Mackenzie na washukiwa 94 wamefikishwa katika Mahakama hiyo kujibu mashtaka 191 yanayohusiana na mauaji.
Wakiwa mahakamani hapo, watuhumiwa hao wamesomewa mashitaka kadhaa yakiwemo ya mauaji, ugaidi na mateso huku ofisi ya Mwendesha Mashitaka ikisisitiza kuwa ina ushahidi wa kutosha wa kuwatia washukiwa hao hatiani.
Mackenzie, anayemiliki kanisa la Good News International Church, alikamatwa Aprili, 2023.
Zaidi ya miili 420 ya watu walioshawishika kushinda bila kula, kama sehemu ya ibada kutoka kwa mchungaji Mackenzie, ilipatikana imezikwa katika msitu wa Shakahola, unaopatikana pwani ya Kenya.
Inaaminika kuwa, Mackenzie na wenzake walishawishi wafuasi wao kushinda njaa na kisha kufa kama ishara ya ‘kumlaki Yesu’.
Pia inasemekana kuwa, kiongozi huyo wa kanisa la Good News International Church, aliwaamuru wafuasi wake wajiue kwa njaa, kwa ahadi ya kufika mbinguni kabla ya mwisho wa dunia.
" Baada ya uchambuzi wa kina wa ushahidi huo, DPP amejiridhisha kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kuwafungulia mashitaka watuhumiwa 95 kwa makosa ya kuua bila kukusudia, kushambulia na kusababisha madhara makubwa mwilini ,”ilisema taarifa ya ofisi ya Mwendesha Mashitaka.
Miili iliyopatikana, ilizikwa katika makaburi ya kina kifupi kwenye eneo la ekari 800, huko Shakahola.
Mabaki ya baadhi ya miili ya wafuasi hao haikuwa na viungo muhimu mwilini, jambo linalochochea zaidi tuhuma za kuendeshwa kwa biashara za viungo vya binadamu ndani ya ibada hiyo.
Kwa mujibu wa wapelelezi kutoka idara inayoshughulikia kesi za mauaji nchini Kenya, Mackenzie na wenzake walianza kuchimba makaburi ya halaiki kwa ajili ya watu waliopoteza maisha kutokana na ibada hiyo.
Mnamo Aprili 19, 2023, wapelelezi hao walimkuta muathirika mmoja akiwa amezikwa yu hai, huku taarifa na siri za uwepo wa makaburi mengine ya aina hiyo zikizidi kufichuka.
Baadhi ya waumini walikutwa wakiwa wamedhoofika, na wengine kupoteza maisha wakiwa wanakimbizwa hospitalini, katika operesheni maalumu iliyoendeshwa na polisi ndani ya msitu wa Shakahola.
Makaburi yenye vina vifupi, yaligunduliwa katika Kaunti ya Kilifi na uchunguzi zaidi ulibaini mengi zaid katika eneo hilo.
Washukiwa hao watafikishwa katika mahakama ya Shanzu mjini Mombasa Alhamisi ijayo, kujibu tuhuma za ugaidi.