Wavuvi nchini Tanzania wakianza safari yao ya uvuvi katika Bahari ya Hindi mjni Bagamoyo. / Picha: Reuters

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Kenya imeonya wakazi wa maeneo hayo kuwa waangalifu, huku ikitabiri upepo mkali na wastani kuanza Jumanne, Mei 21 hadi Jumatatu, Mei 27 2024.

Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya Dk David Gikungu alisema kuwa upepo wa Kusini-Mashariki wa kati ya noti 10-30 unatarajiwa katika bahari ya Kenya; na urefu wa mawimbi kuanzia mita 1.5 hadi 3.6.

Wanabaharia katika eneo la Pwani ya Kenya wamehimizwa kukwepa maeneo ya kina kirefu cha bahari.

"Upepo mkali watarajiwa katika bahari ya Somalia wenye kasi ya 30 (15 m/s). Kadhalika mawimbi makali yanatarajiwa Somalia, Kenya na Tanzania katika kipindi chote cha utabiri,” Dk. Gikungu alisema

Idara ya MET iliongeza kuwa mvua itaendelea kunyesha Magharibi mwa Kenya, Kaskazini Magharibi, na Bonde la Ufa.

Aidha idara hiyo pia imetabiri mvua za mara kwa mara katika mikoa ya Pwani na kaskazini-mashariki mwa Kenya.

Hali kadhalika Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewashauri wananchi na mabaharia kuwa waangalifu; na kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa.

Taasisi hiyo ilionya ya kwamba kimbunga hicho kitasababisha upopo mkali baharini unaozidi kasi ya kilomita 40 kwa saa na mawimbi yanayozidi mita 2. Huku ikionya kunyesha kwa mvua kali katika maeneo ya pwani kati ya Jumanne 21 Mei na Jumatano 22 Mei.

Hii inakuja baada ya mafuriko makali yaliyoshuhudiwa nchi za Afrika Mashariki hivi karibuni yaliyosababisha vifo na hasara kubwa ya mali na uharibifi wa miundombinu haswa katika nchi ya Kenya na Tanzania.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika