Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeamua kuongeza muda wa kikosi chake cha kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa mwaka mmoja zaidi huku mapigano yakiendela katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Kikosi cha SADC katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMIDRC) kilitumwa mwaka 2023 kusaidia azma ya serikali ya DRC kurejesha amani na usalama mashariki mwa DRC.
Taarifa iliyotolewa Jumatano mwishoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi za SADC uliofanyika Harare, Zimbabwe, ilibainisha kuongezeka kwa uhasama mashariki mwa DR Congo.
“Tuna wajibu wa kuimarisha azma yetu na kupanga njia ya kusonga mbele ambayo itatuwezesha kushinda vita hivi kwa amani na haki ya watu wa Mashariki mwa DRC kwa maisha bora na ustawi, maendeleo, haki pamoja na taasisi imara," amesema Rais wa Zimbabwe na Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC, Emmerson Mnangagwa.
Viongozi wa SADC walisema uamuzi wa kuongezwa muda kwa kikosi cha kulinda amani ni muendelezo wa "mwitikio wa kikanda kushughulikia hali ya usalama isiyo na utulivu iliyopo mashariki mwa DRC."
Viongozi wengine wanne wa nchi kutoka Botswana, DR Congo, Madagascar na Msumbiji, walihudhuria mkutano huo, wakati viongozi wengi kutoka kundi la kikanda lenye wanachama 16 walituma wawakilishi.
Taarifa ya mkutano huo pia imekaribisha juhudi zinazoendelea za Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kuchunguza chaguzi mbalimbali za kuunga mkono SAMIDRC.
Mapema mwaka 2023, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilipeleka jeshi la kikanda katika eneo lililokumbwa na migogoro, na kusababisha kusitishwa kwa mapigano kuanzia Machi hadi Septemba 2023.
Hata hivyo, Disemba mwaka huo, serikali ya DRC ilikataa jeshi la kikanda la EAC na nafasi yake ikachukuliwa na kikosi cha mani cha SADC.
Jeshi la Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) lilikamilisha kuondoka kutoka Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini DRC tarehe 21 Disemba 2023.