Bunge la Kenya lilipiga kura siku ya Jumanne kumshtaki Gachagua kwa mashtaka 11 yakiwemo kujitajirisha na kuchochea chuki za kikabila. / Picha: Reuters

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa kesi ya kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ipelekwe kwa Jaji Mkuu kwa mwelekeo zaidi.

Kikosi cha mawakili wa Gachagua, kikiongozwa na Wakili Mkuu Paul Muite, Jumatano kilisema kuwa kesi hiyo inaibua masuala muhimu ya kikatiba, kwani ndiyo ya kwanza inayohusisha kuondolewa kwa Naibu Rais.

"Masuala haya yanaibua swali kubwa la sheria. Inabidi Mahakama Kuu ipeleke kesi hii kwa jaji wa Mahakama Kuu ili kuunda Tume ya Majaji ya kusikiliza kesi hii," Muite aliiambia Mahakama Kuu.

Bunge la Kenya lilipiga kura siku ya Jumanne kumshtaki Gachagua kwa mashtaka 11 yakiwemo kujitajirisha na kuchochea chuki za kikabila. Naibu Rais alikanusha madai hayo yote na kusema kuwa kesi hiyo ni ya kipuuzi.

Bunge la Seneti wiki ijayo litajadili mashtaka hayo na kupiga kura ya kumuondoa ofisini.

Jaji Lawrence Mugambi wa mahakama kuu alisema maslahi ya umma katika kesi hiyo yanahitaji kuundiwa jopo la majaji kuchunguza ombi la Gachagua.

Kujitetea kwa seneti

Baada ya bunge la kitaifa kupiga kura kumuondoa madarakani kesi ya Gachagua ilipelekwa kwa Bunge la Seneti.

Seneti sasa imetoa mpango kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Alhamisi, Oktoba 17, afike mbele ya maseneta ili kujitetea kwa saa 4 .

Kutoka saa tatu za asubuhi hadi saa saba mchana Gachagua atawasilisha ushahidi wake dhidi ya sababu za kushtakiwa halafu seneti itakuwa na kikao kingine alasiri kwa mahojiano.

Katika kipindi hicho, mawakili wa Gachagua pia watakuwa na nafasi ya kuwaita mashahidi kwenye mkutano huo, ambao wanaamini watasaidia kuokoa kazi yake.

Timu yake ya wanasheria inasema wana mashahidi kadhaa waliojipanga lakini hawakufichua majina yao.

Baada ya uwasilishaji wake, Maseneta watapata nafasi ya kuhoji na kutafuta ufafanuzi kutoka kwa Naibu Rais mwenyewe kabla ya kuikaribisha timu yake kutoa mawasilisho yao ya mwisho kwa muda wa saa moja.

TRT Afrika