Rais William Ruto amewataka Wakenya wanaoishi katika ardhi ya serikali kinyume cha sheria lakini wapo tayari kununua ardhi hiyo kwa bei ya thamani ya soko, kufanya hivyo ili kuepusha kubomolewa na hatimae kupoteza nyumba zao.
"Wale ambao wana uwezo wacha wakubaliane malipo na waendeleee kuishi hapo," rais Ruto amesema.
Rais alisema hayo alipokuwa katika mkutano na maafisa wa elimu, jijini Nairobi.
Matamshi yake yanajiri baada ya kubomolewa kwa nyumba, makanisa, shule na majengo ya biashara katika eneo lenye ekari 4000, Kusini Mashariki mwa jiji la Nairobi.
Hiyo ilitokana na uamuzi wa mahakana ambayo iliamua kuwa kampuni ya saruji ya East African Portland Cement (EAPCC) ndiyo mmiliki halali wa shamba la ekari 12,000 na hivyo kuwalazimisha watu waliokuwa wanaishi hapo muda mrefu kuhama.
Hata hivyo, rais Ruto amesema kuwa watu wanaomiliki ardhi yoyote ya umma watalazimika kulipa serikali kwa bei ya ardhi ya soko ya sasa.
" Lakini wale ambao wanataka kutumia ulaghai na kuleta vyeti vya kudai ardhi ni yao ilhali ni vyeti bandia, hiyo haitakubalika," Ruto amesema
"Tunahitaji pesa kujenga viwanda vyetu, hivyo basi, walio katika ardhi za serikali watulipe pesa waendelee na maisha yao ama kama si hivyo, mambo tu ni yale yale,(waondoke)." ameongezea.