Wizara ya ndani imetoa ilani kwa NGOs nchini kuainisha shughuli zao na kutoa vipaumbele kwa maendeleo ya Kenya kama ilivyoainishwa katika ajenda ya Serikali / Picha : X - Wizara ya Ndani 

Serikali ya Kenya imeyaonya mashirika yasiyo y akiserikali - NGO- yanayoendesha shughuli na miradi ya kimaendeleo nchini humo, kuainisha utendaji wao sambamba na ruwaza ya utawala wake.

Kupitia taarifa kutoka wizara ya ndani, Serikali ya Kenya imeeleza kuwa, ingawa inatambua mchango na msaada wa mashirika hayo kwa nchi hiyo, ni lazima yawajibike ipasavyo pamoja na mataifa yanayoyafadhili kwa kuzingatia kanuni zinazofaa za kimataifa za operesheni zao.

Wizara ya ndani imeeleza kuwa imetoa ilani rasmi kwa mashirika hayo na mashirika ya manufaa ya umma (PBOS) nchini kuainisha shughuli zao na kutoa vipaumbele kwa maendeleo ya Kenya kama ilivyoainishwa katika ajenda ya 'BETA' Bottom-Up Economic Transformation Agenda yaani Mabadiliko ya Kiuchumi ya Chini-Juu kulingana na mipango ya rais William Ruto.

"Tunatambua jukumu muhimu la misaada ya wafadhili katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi, lakini, usanifu wa misaada lazima uzingatie kanuni bora za kimataifa na mifumo ya udhibiti iliyowekwa." Wizara ya ndani ilisema.

"Kufuatia tathmini yetu ya utendakazi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na Mashirika ya manufaa ya umma (PBOS) yaliyosajiliwa nchini Kenya, Serikali imegundua kwa wasiwasi, upotoshaji uliopo wa mifumo ya kimataifa ya usimamizi wa misaada ya wafadhili." Taarifa ilieleza.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa Raymond Omollo, imeonekana kuyaondolea mashirika hayo hofu na kusema kuwa lengo lake kuu ni kuimarisha thamani ya miradi yote inayofadhiliwa kupitia misaada ya kimataifa ili kuhakikisha inakamilisha mipango ya maendeleo ilyioainishwa katika mfumo wa BETA.

TRT Afrika