Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ikiwa katika moja ya vikao vyake jijini Arusha, Tanzania./Picha: EACJ

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Mwanasheria kutoka Uganda, Hassan Mabirizi ameishtaki serikali ya Kenya katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kufuatia kuondolewa kwa Peter Mathuki kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivi karibuni.

Katika kesi namba 14 ya 2024, iliyofunguliwa jijini Arusha, Tanzania, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Mabirizi anadai kuwa uamuzi wa Rais William Ruto wa kumpangia Mathuki majukumu mengine, kama balozi wa Kenya nchini Urusi, ni ukiukwaji mkubwa wa Ibara ya 67(4) ya itifaki ya uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, Katibu Mkuu wa EAC, anapaswa kuhudumu kwa kipindi cha miaka 5. Hata hivyo, Mathuki alikuwa amehudumu kwa miaka 3, katika nafasi hiyo ya juu ndani ya EAC, kabla ya maamuzi ya Machi 8, yaliyofikiwa na Rais Ruto.

Aliyekuwa Katibu Mkuu, Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki | Picha: EAC

Katika kesi hiyo, Mabirizi ameiomba mahakama ya EACJ kumuwekea pingamizi Rais Ruo, kuteua mbadala wa Mathuki ndani katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hivi karibuni, Rais Ruto alimteua Caroline Mwende Mueke, kama mbadala wa Mathuki ndani ya EAC, akitarajiwa kumalizia kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa mtangulizi wake ambaye kwa sasa ataiwakilisha Kenya kama balozi nchini Urusi.

Kulingana na itifaki ya kuanzisha EAC, Rais wa nchi husika anaweza kupendekeza jina kwa nafasi ya Katibu Mkuu, kabla ya kuidhinishwa na Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki.

Nafasi hiyo huwa ni ya mzunguko kwa kila nchi mwanachama, na mteule huhudumu kwa muda wa miaka mitano.

"Mlalamikaji, anaitaka EACJ kubatilisha maamuzi ya Machi 8 ya Rais William Ruto ya kumuondoa Mathuki katika nafasi ya Ukatibu Mkuu wa EAC, wakati muda wake bado haujaisha," imesomeka sehemu ya hati ya mashtaka hayo.

Rais William Ruto amemtua Caroline Mwende Mueke kutoka Kenya, kama mbadala wa Mathuki katika Sekretarieti ya EAC./Picha: Wengine

Hali kadhalika, Mabirizi ameituhumu Kenya kwa kudharau dhana ya Utawala wa sheria na fursa sawa, ambayo ni kanuni ya msingi ya EAC kama ilivyoanishwa katika Ibara ya 6(d) na Ibara ya 7(2) ambayo inaangazia Utawala wa Sheria kama msingi wa kuendesha shughuli za kila siku ndani ya Jumuiya hiyo.

Hata hivyo, Kenya haijatoa kauli yoyote kuhusu kesi hiyo.

TRT Afrika