Jaji wa Mahakama kuu Kenya Daniel Ogembo Ogola amefariki / Picha: Wengine 

Jaji wa Mahakama kuu Daniel Ogembo Ogola amefariki. Gavana wa Kaunti ya Siaya James Orengo alitangaza kuaga kwa jaji huyo mnamo Jumatano, Julai 17.

“Naungana na mahakama kote nchini kuomboleza kifo cha Mhe. Jaji Daniel Ogembo Ogola ambaye alikuwa Jaji msimamizi katika Mahakama Kuu ya Siaya, “ gavana wa Siaya James Orengo amesema katiak taarifa.

Mwili wa jaji huyo mashuhuri ulipatikana nyumbani kwake katika kaunti ya Siaya.

Maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha kifo cha hakimu huyo.

Tangazo hilo lilitolewa huku wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wanasheria wa karibu walikuwa bado kwenye mazishi ya marehemu ya Jaji wa mahakama kuu David Majanja.

Majanja alifariki Juni 11, baada ya kufanyiwa upasuaji uliofanikiwa.

Marehemu David Majanja aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu mwaka wa 2011. Alipoteuliwa, alihudumu katika Mahakama Kuu za Homa Bay, Migori, Kisumu na Kisii. Aidha, Majanja alihudumu katika Kitengo cha Biashara na Ushuru na Kitengo cha Kiraia katika Mahakama Kuu ya Milimani.

Katika kisa tofauti, Hakimu Mkuu wa Makadara jijini Naiorbi, Monica Kivuti alifariki Juni 2024, baada ya kupigwa risasi na afisa wa polisi ndani ya chumba cha mahakama.

Kivuti alifariki baada ya kupigwa risasi kifuani na kiunoni na Inspekta OCS wa Londiani Samson Kipruto wakati wa katika kikao mahakamani.

TRT Afrika