Rais William Ruto ametia saini Mswada wa Ubinafsishaji, 2023 kuwa sheria / Picha ya Ikulu ya Kenya

Rais wa Kenya William Ruto ametia saini Mswada wa Ubinafsishaji, 2023 kuwa sheria.

Sheria hii inaondoa urasimu katika ubinafsishaji wa mashirika ya umma yasiyo ya kimkakati au yanayoonekana kuwa ya hasara.

Mswada huu unahimiza ushiriki zaidi wa sekta binafsi katika uchumi kwa kuhamisha uzalishaji na utoaji wa bidhaa na huduma kutoka kwa sekta ya umma.

Baraza la mawaziri mnamo tarehe 22 mwezi Machi, 2023, uliidhinisha mswada mpya wa ubinafsishaji ambao utahusisha mali ya serikali kuuzwa kwa sekta binafsi kupitia masoko ya mitaji ya nchi.

"Sheria iliyokuwepo hapo awali ilifanya iwe vigumu kwa Wakenya kumiliki kipande chochote cha mali ya Kenya," rais willima Ruto alisema, "kukiwa na sheria mpya tunaweza kuweka demokrasia kwa utajiri wetu na kuruhusu mkenya kumiliki kipande cha kile ambacho ni cha nchi yake."

Sheria hii mpya inalenga kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma za umma kwa kushirikisha mtaji na utaalamu binafsi.

Katika hatua hii mpya, ubinafsishaji utafanywa kwa njia ya awali ya kutoa hisa kwa umma, uuzaji wa hisa kwa zabuni ya umma.

Pia itahusisha uuzaji unaotokana na utekelezaji wa haki za awali au kwa njia nyengine yoyote itakayofafanuliwa na baraza la mawaziri.

Mswada huo unaeleza kwamba mapato kutokana na mauzo ya hisa za Serikali ya Kitaifa ya moja kwa moja yatalipwa katika hazina ya pamoja.

Tume ya ubinafsishaji ya Kenya imetaja makampuni 25 yanayolengwa kwa ajili ya ugawaji wa fedha za serikali.

Makampuni hayo ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kenya, Shirika la Agrochemical and Food Corporation, Mamlaka ya Bandari ya Kenya, Kampuni ya Mafuta yani Kenya Pipeline Company na makampuni kadhaa ya sukari.

Mswada huu unakuja wakati ambapo kuna wimbi la wakenya wanaopinga hatua hiyo, kwa madai kwamba huenda utekelezaji wake usiwanufaishe walio wengi.

Wakati huo huo, kuna baadhi wanahisi hatua hiyo, italeta ufanisi mkubwa baada ya baadhi ya mashirika hayo kushindwa kujiendesha kwa faida.

TRT Afrika