Serikali ya Kenya imesema inachunguza jinsi kiongozi maarufu wa upinzani nchini Uganda Kiiza Besigye alivyoondolewa Nairobi wiki hii, huku kukiwa na ukosoaji mkubwa kwamba serikali imeshindwa kuwalinda wapinzani wa kigeni katika ardhi yake.
Kizza Besigye, mpinzani wa muda mrefu wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, inadaiwa kuwa alitoweka katika mji mkuu wa Kenya siku ya Jumamosi.
Besigye alionekana tena siku ya Jumatano akiwa katika Mahakama ya Kijeshi katika nchi jirani ya Uganda, ambako alishtakiwa kwa makosa kadhaa ikiwemo ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Msemaji wa serikali ya Uganda alisema siku ya Jumatano haikufanya utekaji nyara na kwamba ukamataji nje ya nchi ulifanyika kwa ushirikiano na nchi mwenyeji.
Lakini Kenya inakana
Katika mahojiano ya televisheni Jumatano jioni, Korir Sing'oei, Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, alisema kuzuiliwa kwa Besigye - ambako alitaja kama utekaji nyara - "sio kitendo cha serikali ya Kenya."
Sing'oei alisema bado hana ukweli wote, lakini alisema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imeanza uchunguzi kuhusu jinsi Besigye "alivyoondolewa kwa nguvu kutoka majengo ya nchi yetu na kupelekwa Uganda."
"Dkt. Besigye ni mgeni wa mara kwa mara; anakuja hapa kibinafsi kufanya biashara na shughuli kibinafsi. Ninachofahamu kuna itifaki wakati mwengine zinazohusiana na safari ya viongozi wakuu wa serikali na upinzani," Korir alisema.
"Mara nyingi, wanatujulisha uwepo wao katika nchi zetu, wanaweza kutafuta usaidizi maalumu kwenye viwanja vya ndege na kwa msingi huo tunaweza hata kuwapa usalama."
Katika kesi ya Besigye hata hivyo, Singoei alidai serikali haikufahamishwa kuhusu ziara yake Nairobi, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa mamlaka za mitaa kurahisisha safari yake na kutoa usalama zaidi.
“Mazingira ya safari yake hatuyafahamu kwa sababu hakuna taarifa yoyote tuliyoshirikishwa kabla hajasafiri, hatujui alipangiwa hoteli gani wala aliishi ghorofa gani na hivyo hatukuwa na uwezo wa kumpatia usalama wa ziada," alisema Katibu Mkuu.