Kenya imeapisha majaji 20 wapya / Picha kutoka Judiciary Kenya

Rais William Ruto amesema serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za sekta ya sheria. Rais ameapisha majaji wapya 20 wa Mahakama Kuu.

"Tutatoa mchango wetu ili kuimarisha uwezo wa Mahakama katika kutoa haki katika kila sehemu ya Kenya, hasa kupitia miradi ya maendeleo ya miundombinu," Rais Ruto alisema.

Kati ya majaji wapya hao 20, wanane ni wanawake.

Majaji wa Mahakama Kuu waliteuliwa baada ya majina yao kupendekezwa na Tume ya Huduma ya Mahakama ya Kenya, baada ya mahojiano ya watu zaidi ya 80 kufanyika kati ya Aprili 3 na Mei 3 mwaka 2024.

Wakati huo huo, Rais Ruto aliwataka majaji hao kukataa aina yoyote ya ufisadi na kuwatumikia Wakenya kwa uadilifu na weledi.

"Ninawahimiza kujitolea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na weledi, na kukataa rushwa katika kila dalili zake," alisema.

Ufadhili wa sekta ya haki na sheria na utaratibu ili kukabiliana na ufisadi na kukuza uwajibikaji umeongezeka kutoka zaidi ya dola milioni 650 ( shilingi bilioni 87) hadi zaidi ya dola milioni 800 ( shilingi bilioni108 bilioni) tangu mwaka wa kifedha wa 2022/23.

Tume ya Huduma ya Mahakama ya Kenya imesema majaji hawa wapya watachangia vikubwa kupunguza idadai ya kesi mingi .

Kwa sasa Kenya ina majaji 78 ambao wanahudumu katika vituo 45 nchini kote.

Mpango wa Matokeo ya Haraka

"Majaji wapya waanza Mpango wa Matokeo ya Haraka (yaani Rapid Results Initiative, RRI) katika vitengo saba vya Mahakama Kuu katika Mahakama za Sheria za Milimani ili kutatua kesi 120,000 ndani ya miezi sita ijayo," Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome amesema,

"Tunalenga mahakama katika eneo pana la Nairobi, ambalo linachukua asilimia 30 ya mrundikano wa kesi za kitaifa, kwa lengo la kusuluhisha kesi 9,417 za ziada," ameongezea.

Jaji Mkuu Koome anasema kufikia tarehe 30 Machi 2024, jumla ya kesi zilizokuwa zikisubiriwa katika Mahakama Kuu zilikuwa 68,121. Hii ina maana kwamba kila jaji atakuwa na mzigo wa kesi 873.

Majaji hao wapya pia watasaidia katika mchakato wa kupunguza idadi ya wafungwa waliojaa kupita kiasi katika magereza.

"Kufikia jana (13 mei 2024) magereza yetu yalikuwa yanawashikilia wafungwa 62,639, ambao wanazidi kiasi kinachohitajika cha 30,000. Tunalenga kukagua hukumu kwa wale waliopatikana na hatia kwa makosa madogo ili kupunguza idadi ya wafungwa kwenye vituo," Jaji Koome ameongeza.

TRT Afrika