Wabunge wa Kenya wameahidi kuweka sheria mpya zitakazoadhibu uhalifu wa wizi wa mifugo sawa na kosa la Ugaidi.
Wabunge hao walitangaza pendekezo hilo baada ya ziara rasmi ya kiserikali ya kuchunguza hasara zinazotokana na wizi wa mifugo ikiwelo vifo.
"Tunazingatia kama bunge kujumuisha vitendo vya wizi wa ng'ombe na ujambazi pamoja na ugaidi ili yeyote atakayepatikana na hatia ya kujihusisha na vitendo hivyo atakabiliwa na nguvu ya sheria," alisema mwenyekiti wa kamati ya idara ya utawala na usalama wa ndani Gabriel Tongoyo baada ya ziara hiyo.
Hata hivyo, wataalamu wa sheria wanashauri kuwa kuongeza vipengele vipya au kuunda sheria mpya za kukabiliana na uhalifu ambao tayari una sheria zinazosimamia sio jibu.
''Kunazo sheria tayari ambazo zinasimamia uhalifu wa aina hii, ikiwemo adhabu zinazostahiki,'' anasema Robert Muigai, mwanasheria jijini Nairobi. 'Nadhani ni muhimu zaidi kuhakikisha utekelezaji wa sheria unafanyika kikamilifu kwani chochote wanachotaka katika sheria mpya tayari kimeangaziwa na sheria zilizopo,'' anaongeza.
Hata hivyo Mbunge wa Narok Kaskazini, eneo ambalo limeathiriwa kwa muda mrefu na tatizo la wizi wa mifugo, Gabriel Tongoyo, amesisitiza kuwa wizi wa mifugo lazima ukomeshwe kwa namna moja au nyingine.
''Kutokana na wa idadi ya vifo vinavyoonekana, na uharibifu wa mali, wizi wa ng'ombe hauwezi kuendelea kuchukuliwa kwa wepesi,'' aliongeza bwana Tongoyo.
Sheria na tathmini zake
Kwa mujibu wa kamati ya bunge, zaidi ya watu 600 wameuawa wakati wa kipindi cha uchaguzi uliopita kutokana na visa vya wizi wa mifugo.
Unapotizama sheria ya aina yoyote lazima kuna tathmini ya sheria hiyo, muktadha wake unapotumika na mazingira ya shitaka.
Na tafsiri ya sheria inazingatiwa kwa kanuni tatu muhimu zikiwemo kanuni halisi (literal rule) kanuni ya dhahabu (golden rule) na sheria ya utundu ( Mischief rule)
''Kanuni inayotyumika hapa ni Mischief rule, ambayo ni uhalifu gani au utundu wa aina gani unaweza kuponywa kwa kutumiwa sheria hii. Na hapa watakuwa wanalenga kudhibiti wizi wa mifugo,'' anasema Robert,
Lakini Robert anashauri kuwa, hakuna haja kuweka majin amakubwa au mazito yanayotoa vitisho zaidi ili kuhakikisha sheria inatekelezwa.
''Ukitazama mfano sheria ya mauaji ipo, na mauaji ya kusudi bila sababu muafaka inapewa hukumu hata ya maisha jela. Lakini haina maana kuwa mauaji yametokomezwa. Bado watu wanaua,'' amesema Robert.
Wabunge kutoka eneo la kaskazini mwa nchi waliipongeza serikali kwa mpango wake wa kijeshi ambao unatilia nguvu kufunguliwa kwa barabara na ujenzi wa shule za bweni katika eneo hilo ili kutoa elimu kwa watoto hasa kutoka katika jamii za wafugaji jambo ambalo alisema litapunguza uwezekano wa watoto kuingizwa katika vitendo hivyo haramu.
Hata hivyo wabunge hao hawajabainisha ni lini watawasilisha miswada hiyo bungeni ili kujadiliwa.