Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Profesa Kithure Kindiki: Picha: Kithure Kindiki

Serikali ya Kenya kupitia wizara yake ya mambo ya ndani imefuta nyongeza ya malipo, tozo na ushuru za stakabadhi muhimu baada ya kuibua hisia miongoni mwa Wakenya.

"Ilani ya Gazeti la serikali la tarehe 7 Novemba 2023 imefutwa ili kuruhusu ushiriki zaidi wa umma juu ya suala hilo," Waziri Kithure Kindiki aliandika kwenye ukurasa wake rasmi kwenye mtandao wa X.

Juma lililopita, serikali hiyo kupitia gazeti kuu la serikali ilitangaza nyongeza ya ada zilizotozwa huduma mbalimbali za idara za uhamiaji na huduma za raia.

Wakenya wangehitajika kulipa ada zaidi kupokea au kubadili stakabadhi muhimu kama vile vitambulisho vy akitaifa na pasipoti chini ya idara ya uhamiaji katika ada mpya zilizotangazwa na serikali.

Hata hivyo siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya ndani Profesa Kithure Kindiki ametangaza kufutilia mbali tathmini ya ada hizo.

"Ada mpya, na malipo ya hivi majuzi, yamerekebishwa ili kukidhi maoni ya umma ambayo tayari yamepokelewa kufuatia kuchapishwa kwa matangazo ya Gazeti ya serikali," Waziri Kindiki alitangaza.

Serikali imekarabati ada mpya ya kitambulisho, kwa raia wasiosajiliwa awali, kutoka shilingi 1,000 hadi shilingi 300.

Hata hivyo, wizara hiyo imesema serikali itawasemehea tozo Wakenya watakaoonyesha kutokuwa na uwezo wa kulipa kwa kugharamia tozo yenyewe.

Aidha, ada ya kitamulisho kilichopotea imepunguzwa kutoka shilingi 2,000 hadi shilingi 1000 baada ya kuzua gumzo nchini humo.

Hata hivyo, ada za pasipoti za kawaida zenye kurasa 34 zimesalia na nyongeza ya awali ya ada kutoka dola 30 hadi dola 50.

Tozo za kubadilisha pasipoti iliyopotea imesalia ilivyokuwa na itagharimu shilingi 20,000.

Kwa sasa, idara husika za uhamiaji na huduma za raia zimepewa hadi tarehe 10 Desemba 2023 huku zikielekezwa kufanya na kukamilisha ushiriki wa umma haraka iwezekanavyo.

TRT Afrika