Kithure Kindiki aliyependekezwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani. Mwanasiasa huyo amewahi kushikilia nafasi hiyo kabla ya Rais William Ruto kutengua baraza lake lote mwezi Julai, 2024./Picha: Bunge la Kenya             

Bunge la Kenya limeanza kuwahoji na kuwachunguza wateuliwa kwenye Baraza la Mawaziri lililotangazwa hivi karibuni.

Rais William Ruto amependekeza majina ya watu 21 wanaotegemewa kuongoza Wizara mbali mbali, akiwemo na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo.

Kamati hiyo inaongozwa na Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetangula.

" Tunapoanza vikao vya kuidhinisha Wateule wa baraza la mawaziri , ninataka kuwahakikishia wananchi wa Kenya kwamba Kamati ya Uteuzi itachunguza kwa kina kila wasilisho lililotolewa," alisema Wetangula.

" Endapo mawasilisho yaliyopokelewa hayako katika mfumo wa hati za kiapo kama inavyotakiwa kisheria, kamati, kadiri inavyowezekana itajumuisha hoja kupitia maswali kwa wateule," spika huyo ameongeza.

Wa kwanza kuhojiwa katika mchakato huo, amekuwa ni Kithure Kindiki ambaye amependekezwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani. Mwanasiasa huyo amewahi kuiongoza Wizara hiyo kabla ya Rais Willim Ruto kutengua baraza lake lote mwezi Julai, 2024.

Moses Wetangula Spika wa Bunge la nchi hiyo anaongoza kamati ya kuhoji waliopendekezwa kuwa Mawaziri./Picha:  Bunge la Kenya 

" Nilipofika ofisini, hati za kusafiria zilikuwa ndoto lakini leo tumelipa madeni yote tumeongeza mfumo wa ICT na kuondoa msongamano na tulikuwa tukitoa pasipoti za kusafiria ndani ya siku 7," alisema Kindiki, wakati akijetetea mbele ya Kamati ya ili apewe fursa nyingine ya kuongoza Wizara hiyo.

" Wakati naondoka madarakani, kulikuwa na mpango kwamba ifikapo Novemba mwaka huu tupunguze muda wa kusubiria pasipoti iwe ndani ya siku 3. Tunashughulika watumishi wafisadi ili kusafisha kila mahali," Kindiki aliongeza.

Wizara ya mambo ya ndani ilipata changamoto kubwa hasa wakati wa maandamano ya Gen Z, huku Polisi wakilaumiwa kwa matumizi ya nguvu za ziada, zilizosababisha vifo vya watu 50 na mamia wengine kujeruhiwa wakati wa maandamano ya amani.

Kuhusu suala la sheria na utulivu wakati wa maandamano ya amani, Prof Kindiki alikiri kuwepo kwa mapungufu, akiahidi kuwa iwapo jina lake litapitishwa, atahakikisha kwamba watu wa Kenya wanafurahia uhuru wao na wakati huo huo kudumisha utulivu wa umma.

Mchakato huo wa 'uhakiki na uchunguzi', pia utahusisha waliopendekezwa kwenye nafasi za Wizara za Afya, Ardhi , Elimu na Usalama.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

TRT Afrika