Miili ya wafuasi wa kanisa la Good News International, iliyokuwa imezikwa katika msitu wa Shakahola pwani mwa Kenya ikifukuliwa / Picha: Reuters

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya, Kithure Kindiki ameliita kanisa la Good News International Ministries kama kikundi cha kihalifu.

Tamko hilo limetolewa na kupitia tangazo la gazeti la Serikali.

Kanisa hilo, lililoanzishwa na Paul Mackenzie mwaka 2003, linahusishwa na vifo vya watu zaidi ya 427, katika msitu wa Shakahola unaopatikana katika eneo la pwani ya Kenya.

Hapo awali, Waziri Kindiki aliazimia kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote aliyeshiriki kwenye mauaji hayo.

Januari 2024, Mahakama nchini Kenya ilimshtaki kiongozi huyo wa 'ibada ya njaa' na wenzake 94 kwa ugaidi na kuua bila kukusudia na hivyo kusababisha vifo vya zaidi ya watu 400.

Mackenzie aliwashawishi wafuasi wake kushinda njaa ili 'wamuone Yesu'.

Kulingana na uchunguzi uliofanyika kwenye miili mingi ya waathirika hao, asilimia kubwa ya watu walikufa kwa njaa.

Uchunguzi huo ulibaini kuwa makundi ya watoto walipoteza uhai kutokana na kunyongwa ama kupigwa.

Waathiriwa 238 waliotajwa katika kesi ya Jumanne waliuawa "katika tarehe isiyojulikana kati ya Januari 2021 na Septemba 2023 huko Shakahola," hati za mahakama zilisema.

TRT Afrika