Renson Ingonga atahudumu kuwa Mkurugenzi mkuu mpya wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya kwa kipindi cha miaka minane.
Uteuzi huo ulifanywa kupitia tangazo rasmi la gazeti kuu la taifa.
"Katika utekelezaji wa madaraka yaliyotolewa na Ibara ya 157 (2) ya Katiba na kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa chini ya kifungu cha 8 (8) Cha Sheria ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, 2013, namteua Renson Mulele Ingonga Kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma,"
Afisa huyo anajaza pengo lililoachwa na Noordin Haji ambaye anashikilia wadhfa wa mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kabla ya kuteuliwa na Rais Ruto, wakili Mulele amekuwa akihudumu kama Naibu Mkurugenzi mwandamizi wa Mashtaka ya Umma akisimamia mkoa wa Kaskazini mashariki nchini humo.
Mwezi uliopita, Mulele, aliliambia bunge la Kenya kuwa hatokubali idara yake kuingiliwa kisiasa na kwani ataongozwa na sheria katika utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini Kenya na Ofisi ya Mkurugenzi Wa Uchunguzi Wa Jinai (DCI) zimekuwa zikishuhudia mvutano wa mara kwa mara haswa katika enzi za wakuu waliokuwa wakisimamia ofisi hizo za DCI na DPP hapo awali, George Kinoti na Noordin Haji.
Hata hivyo Mulele ameahidi kufanya kikao na ofisi ya DCI na kutofautisha mamlaka ya kila taasisi.
Kenya imekumbwa na lawama kutoka upinzani kuhusu mwenendo wa hivi karibuni wa kuondolewa kwa kesi za hali ya juu kwa madai ya ukosefu wa ushahidi na kuchochewa kisiasa licha ya kuwasilishwa na kuanza muda mrefu.
Hivi majuzi, Mulele amefafanua kuwa ataelekezwa na nguvu ya DPP kuondoa kesi mahakamani jinsi ilivyowekwa wazi katika sheria na kwamba mahakama ndio yenye uwezo wa kuthibitisha iwapo sababu zilizotolewa kwa ajili ya kutafuta uondoaji wa kesi ni halali au la.