Madaktari nchini Kenya wamekuwa katika mgomo toka katikati ya mwezi Machi.Picha/AA

Hospitali ya taifa ya Kenyatta imewafukuza kazi madaktari 100 wanaoshiriki katika mgomo wa nchi nzima uliodumu kwa mwezi mmoja sasa, uongozi wa hospitali hiyo ulisema siku ya Jumanne.

Hospitali hiyo pia imetangaza kuajiri madaktari wapya kuchukua nafasi ya wale walioachishwa kazi.

Madaktari nchini Kenya waliingia kwenye mgomo wa nchi nzima kuanzia mwezi Machi, wakishiniza malipo mazuri na uboreshwaji wa mazingira ya kufanyia kazi.

Siku ya Jumapili, Rais William Ruto alivunja ukimya na kuweka wazi kuwa hakuna pesa ya kuwalipa madaktari walioamua kugoma.

“Ni lazima tuwe wakweli, kwamba ni bora tuishi kulingana na uwezo wetu, hatuko tayari kukopa pesa kulipa mishahara”, Ruto alisema.

Umoja wa madaktari wa nchini hiyo walishikilia msimamo wao, ambapo siku ya Jumanne, mamia ya watoa huduma hao walishiriki katika maandamano na kupeleka ombi lao katika bunge la taifa, wakilitaka kuingilia sakata lao.

Hii si mara ya kwanza kwa madaktari nchini Kenya kugoma wakilalamikia malipo duni na mazingira yasiyo rafiki ya kufanya kazi. Mwaka 2017, kulitokea mgomo wa siku 100, ambao ulisababisha wagonjwa kupoteza uhai wao kwa kukosa huduma ya afya. Mgomo huo uliisha baada ya umoja wa madaktari kukubaliana na serikali kuhusu nyongeza ya mishahara yao.

Madaktari hao wanalalamika kuwa sehemu ya makubaliano ya mwaka 2017, hayajatekelezwa.

TRT Afrika
AP