Zaidi ya wanafunzi milioni 1.4 wanaanza mtihani wao wa kitaifa wa KCPE leo nchini Kenya, huku ikiwa mitihani ya mwisho ya mfumo maarufu kama 8-4-4, uliopewa jina hilo kutokana masomo ya miaka 8 shule ya msingi, miaka 4 sekondari na kisha miaka 4 ya chuo.
Kenya imebadilisha mfumo huo baada ya miaka 38, kufuatia malalamiko mbali mbali ikiwemo kwamba mtaala wake hauwajengi wanafunzi kwa misingi ya vipaji na ujuzi wa kiviwanda.
Rais William Ruto alifungua rasmi zoezi la mtihani huu wa kitaifa kwa ziara katika mojawapo ya shule zinazoandaa mtihani.
''Kwa wanafunzi wote wanaofanya mtihani leo, wa KCPE na wale wanaofanyamtihani wa darasa la sita nawatakia kila la heri,'' alisema Rais Ruto alipohutubia wanafunzi.
Mfumo wa zamani pia ulishutumiwa kuwa mzigo mkubwa kupita kiasi kwa wanafunzi ambao walilazimika mara nyingi kusomea masomo mengi kuliko inavyohitajika.
Mfano chini yamfumo wa 8-4-4, mwanafunzi angetakiwa kupita masomo zaidi ya 13 mbali mbali ikiwemo sayansi daraja tatu tofauti na hisabati, lugha, wakati mwingine zaidi ya mbili, ambapo Kiingereza na Kiswahili zilikuwa lazima.
Chini yamfumo huu mpya wa CBC, mtaala unalenga kutambua vipaji vya watoto na kuwapunguzia masomo wanayotakiwa kuchukua kulingana na azma yao na vitengo waliyo na uelewa zaidi.
Pia baadhi ya walimu wamepongeza mfumo huo mpya kwa kuwa unahusisha wazazi zaidi katika masomo ya watoto na sio jukumu la walimu shuleni pekee.
CBC ilizinduliwa nchini Kenya Disemba 2017.