Kenya na Tanzania zimemaliza mgogoro kati yao, unaohusisha kuuziana vifaranga.
Majirani hao kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wameazimia kuendeleza biashara ya kuku kati yao, kwa kuzingatia kufuatwa kwa sheria.
Katika Kikao chao cha siku mbili kilichofanyika kuanzia Aprili 29 hadi 30 katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania, wataalamu wa sekta ya ufugaji na ututoaji wa vifaranga wamesema kuwa kikundi chochote kitakachonuia kusafirisha bidhaa za kuku kati ya nchi hizo mbili kufanya tathmini ya hatari na kuhakikisha kuwa hatua za usafi zinazingatiwa.
“Tumeazimia kuondoa changamoto hizi ili tukuze ustawi wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya,” amesema Dkt Benezeth Lutege Malinda kutoka Tanzania.
Kwa upande wake, Rabson Wanjala kutoka Kenya amesisitiza umuhimu wa kuondoa dosari zinazotawala biashara kati ya nchi hizo mbili.
Mwaka 2017, mamlaka za Tanzania zilichoma moto mzigo uliosheheni vifaranga 6,400 kutoka nchini Kenya, hatua iliyotia dosari uhusiano wa kibiashara baina ya majirani hao.
Vifaranga hao walichomwa moto upande wa Tanzania katika zoezi lililosimamiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Dawa na Chakula nchini Tanzania (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kulingana na mamlaka za Tanzania, uingizwaji wa bidhaa hizo haukufuata sheria na kanuni zilizowekwa.