Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Ushiriki wa Tanzania na Kenya katika mashindano ya Nyika yanayoanza Machi 30, mjini Belgrade, Serbia yameingia dosari baada ya baadhi ya wakimbiaji kukosa viza, ambacho ni vibali maalumu cha kusafiria na kuingia nchini humo.
Maombi ya vibali hivyo yalifanyika Machi 7, mjini Nairobi ulipo ubalozi wa Serbia kwa nchi za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, majibu ya maombi hayo yalitoka Machi 21 ambapo kati ya wanariadha tisa, watano tu ndio waliofanikiwa kupata, katika dakika za lala salama.
Kwa mujibu wa Jackson Ndaweka, ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mchezo wa Riadha Tanzania (RT), kuchelewa kupatikana kwa nyaraka hizo muhimu za safari, kumeifanya timu hiyo kushindwa kwenda Belgrade kushiriki mashindano hayo.
"Tulianza kuomba viza hizo toka Machi 8, lakini mpaka tarehe 21, tulikuwa hatujapata hata moja, hivyo kutulazimu kumtuma muwakilishi wetu kwenda Nairobi kufuatilia suala hilo," amesema Ndaweka.
Kulingana na Ndaweka, vibali hivyo viliombwa kwa matumizi ya wanariadha 8 na mwalimu wao mmoja kwenye mashindano hayo.
"Hadi kufukia sasa, ni viza tano tu ndizo zilizopatikana na muda umezidi kwenda, hatuna budi kuwaruhusu wanariadha wetu warudi majumbani mwao wakapumzike," ameongezeka Kaimu Katibu Mkuu huyo wa RT.
Wakati huo huo, wanariadha watatu kutoka Kenya wameshindwa kuungana na wenzao mjini Belgrade, kwa ajili ya mashindano hayo ya Nyika.
Diana Chepkemoi, Nancy Cherop na Gideon Kipng’etich, watabaki nyumbani baada ya Ubalozi wa Serbia mjini Nairobi kushindwa kuwapa vibali hivyo kwa wakati.
Mkurugenzi wa maendeleo ya vijana katika Shirikisho la Riadha nchini Kenya (AK), Barnaba Korir amesema ubalozi huo umeshindwa kutoa sababu za kushindwa kutoa vibali hivyo kwa wanamichezo hao.
"Limekuwa tatizo kubwa sana hususani kwa nchi zilizoomba viza hizo kutoka ubalozi wa Serbia mjini Nairobi, kwani hadi kufikia Jumatano mchana, vibali hivyo vilikuwa havijatoka," amesema Korir.