AU ATMIS

Kenya na Somalia zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kuundwa kwa kikosi kipya cha usalama nchini Somalia chini ya Umoja wa Afrika, yaani 'AU Led Mission in Somalia', AUSSOM.

Hii ni kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi hizo mbilii baada ya Rais wa Somalia Sheikh Mohamud kukutana na Rais wa Kenya Willim Ruto nchini Kenya.

"Wakuu wa nchi walikaribisha kuanzishwa kwa ujumbe mpya wa Umoja wa Afrika wa kusaidia na kuleta utulivu nchini Somalia, AUSSOM ambao utaendeleza mafanikio ya mtangulizi wake Ujumbe wa Mpito wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS)," taarifa hiyo ya pamoja ilisema.

"Viongozi walikubaliana kuwe na kipindi cha mpito cha majukumu ya usalama kutoka ATMIS hadi AUSSOM ambayo imepangwa kuaza januari 1, 2025," taarifa iliongezea.

Kikosi cha AUSSOM ni kipi?

Agosti 2024, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, liliidhinisha pendekezo la kuunda Ujumbe wa Kusaidia na Kuleta Utulivu wa AU nchini Somalia (AUSSOM).

Itachukua nafasi ya Kikosi cha AU cha Mpito nchini Somalia (ATMIS), ambayo ilichukua nafasi ya ujumbe wa kwanza wa nchi hiyo (AMISOM) mnamo Aprili 2022.

Baraza la Amani na Usalama la Afrika lilisema uamuzi huo ulifuatia

mashauriano kwa ya kina na ATMIS, serikali ya Somalia, Umoja wa Mataifa na washirika wa kimataifa.

Kikosi hicho kinafaa kuingia baada ya hatamu ya ATMIS kuisha mwezi Disemba 2024.

Tayari wanajeshi chini ya kikosi hicho wameanza kuondoka.

Tume ya AU iliahidi katika mkutano huo wa Agosti 2024 kuendelea na mazungumzo ya kina na Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya na washirika wote ili kuhakikisha ufadhili wa kutosha, unaotabirika na endelevu na aina nyingine za usaidizi, kujaza mapengo ya kifedha, kwa AUSSOM.

Nchi gani zitachangia kikosi kipya?

Kikosi cha AU cha ATMIS kinachoondoka nchini Somalia kilichangiwa na nchi kadhaa.

Kwa ombi la Mogadishu, askari 17,500 wa ATMIS wanatarajiwa kuondoka nchini kufikia Disemba 2024.

Nchi zilizochangia katika ATMIS ni zile zile zilizotoa huduma nchini Somalia chini ya ujumbe wa AMISOM tangu 2007.

Uganda ilituma majeshi yake nchini Somalia Machi 2007. Burundi, Ethiopia, Djibouti, na Kenya pia zilituma maafisa wa usalama nchini humo.

Katika kikosi hiki kipya cha AUSSOM, Umoja wa Afrika unatoa wito kwa nchi kujitolea.

"Tunatambua kujitolea kwa Misri na Djibouti kuchangia vipengele vya AUSSOM na kuhimiza nchi nyingine wanachama wa AU katika nafasi ya kufanya hivyo, kuchangia AUSSOM," taarifa ya Baraza la USalama la AU ilisema Agosti 2024.

Septemba 2024, Misri ilituma meli ya kivita na sehemu kubwa ya silaha nchini Somalia zikiwemo bunduki za kukinga ndege na mizinga.

Hii ilipingwa na Ethiopia ambayo ina wanajeshi wake nchini Somalia tangu 2007.

Uhusiano kati ya Somalia na Misri umeonekana kuimarika baada ya Ethiopia na Somaliland kufanya makubaliano ya pamoja Januari 2024, ili kuipa Ethiopia ufukwe wa bahari. Somalia imepinga ikidai kuwa Somaliland iko chini ya Somalia na sio huru kuwa na uwezo wa kufanya makubaliano kama hayo.

Misri kwa upande mwingine imekuwa na mvutano na Ethiopia tangu wakati Ethiopia ilipoamua kujenga bwawa la ukubwa wa zaidi wa Megawati 6000 katika mto Nile.

Misri imekuwa ikidai kuwa Ethiopia haina haki ya kufanya hivyo lakini Ethiopia imesema inahitaji nishati kwa maendeleo ya wananchi wake.

TRT Afrika