Ufukuzi na kutafuta miili iliyozikwa katika msitu wa Shakahola, pwani mwa Kenya unaendelea, huku maafisa wa uslama wakiendelea kutafuta watu ambao wanahofiwa walikufa baada ya kujinyima chakula.
Kiongozi wa ibada ya njaa Paul Mackenzie na wengine wanaodaiwa walimsaidia walikamatwa mwezi Aprili mwaka huu na bado wameshikiliwa huku uchunguzi ukiendelea na wanaedenelea kupelekwa mahakamani.
Mwezi Aprili na Mei, miili 249 na makaburi ya halaiki 10 yamepatikana katika eneo la msitu huo wa Shakahola, wenye ukubwa wa ekari 800.
" Eneo hili ambapo kazi hii ya jinai ya kutisha ilitekelezwa haiwezi kurejeshwa tena kwa shughuli za kawaida za kibinadamu, " Kithure Kindiki, waziri wa mambo ya ndani na utawala wa serikali ya kitaifa amesema.
" Mara tu eneo la uhalifu likiwa wazi na uchunguzi kukwisha na baada ya maelekezo yoyote ya mahakama, eneo la uhalifu litafanywa kama kumbukumbu ya kitaifa," amesema.
Serikali bado inaendelea kufanya uchunguzi wa miili iliyofukuliwa. Waziri Kindiki anasema tayari imebainishwa kuwa kuna watu ambao walinyongwa na wengine kupigwa hadi kufa, hasa wale amabao walionekana kubadili nia yao kuhusu maagizo ya kujinyima chakula.
" Serikali kwa kushauriana na wajumbe na wananchi wa jamii wataligeuza eneo hili la uhalifu kuwa mahali pa ukumbusho ili vizazi vingi vijavyo, karne nyingi baadaye Kenya na ulimwenguni visisahau kulikuwa na aina hii ya ukatili wa binadamu hapa Shakahola," Kindiki amesema.
Waziri anasema kuwa timu yetu ya serikali ina ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka ya mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu, dhidi ya Mackenzie na washirika wake ambao wako rumande.