Tume ya haki KNHCR imesema kuwa mgomo huo umeendelea muda mrefu sana na kutoa wito wa kutafutiwa suluhu ya haraka./Picha Reuters 

Mahakama Kuu nchini Kenya imesitisha agizo la Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome la kuamuru idara za usalama kuwadhibiti wahudumu wa afya wanaogoma ambao alitangaza kuwa maandamano yao ni "kero".

Katika hukumu yake Jumanne jioni, Jaji Jairus Ngaah alitangaza kukomeshwa agizo lililotolewa awali na Inspekta mkuu wa polisi akiwaagiza makamanda wake kuchukua hatua za kuwadhibiti waandamanaji hao, akidai kuwa walisababisha kero kwa umma.

Tamko hilo la Inspekta mkuu lilizua ghadhabu hasa kutoka kwa madaktari wanaogoma, na watetezi wa haki za binadamu wanaodai kuwa linaenda kinyume na haki ya kuandamana na kujieleza ambayo imehakikishiwa chini ya katiba ya nchi.

Vyombo vya kutetea haki za binadamu, kupitia tume ya haki za binadamu nchini Kenya KHRC, ilitoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa vitisho dhidi ya maandamano halali ya kuitaka serikali kushiriki mazungumzo.

''KNHCR inabainisha kuwa kifungu cha 41 cha katiba kinamhakikishia kila mfanyakazi haki ya kuorodheshwa kwa haki, hali nzuri ya kufanya kazi, kujiunga, kuunda au kushiriki katika shughuli za chama cha wafanyakazi na kugoma,'' tume hiyo ilisema katika taarifa yake.

Hata hivyo tume hiyo imesema kuwa mgomo huo umeendelea muda mrefu sana na kutoa wito wa kutafutiwa suluhu ya haraka.

''KNHCR pia inabainisha kuwa mgomo huo umekuwa ukiendelea kwa muda na pande zote mbili zinahitaji kuwa na majadiliano ya kweli kuhusu fomula ya kurejea kazini ili utoaji wa huduma za afya wa kawaida urejeshwe,'' iliongeza tume hiyo.

katika kesi hiyo iliyowasilishwa mahakamani kwa pamoja na watetesi wengine wanane dhidi ya idara ya polisi, tume hiyo ilitaja visa vya ukatili wa polisi kuwa visivyokubalika ikitaja majeraha yaliyoletwa kwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU) Davji Atellah wakati wa maandamano.

Chama cha mawakili nchini Kenya LSK ilisema agizo la Inspekta Koome halina msingi wa kisheria na utunzaji wa ustawi wa umma.

Inspekta huyo amepewa muda wa siku saba kuwasilisha tetesi zake.

Mgomo huo ulioanza Machi 14, umekuwa na athari kubwa kwa mfumo wa huduma za afya, huku hospitali zikilazimika kuwafukuza wagonjwa au kufanya kazi na wafanyikazi na rasilimali chache.

Licha ya hayo, kumekuwa na vuta nikuvute kati ya waziri wa afya Susan Nakhumicha na wawakilishi wa muungano mbali mbali za wahudumu wa afya, ambapo wakayi mwingine mikutano imekatishwa ghafla kwa kujiondoa waziri kutokana na kutoelewana.

TRT Afrika