Rais wa Kenya, William Ruto amevunja mkataba na kampuni ya Adani. / Picha: AFP

Rais William Ruto katika hotuba yake kwa taifa ya kila mwaka alitangaza ya kuwa serikali yake imebatilisha mikataba miwili na kampuni ya Adani. Haya yanajiri baada ya wafanyakazi katika viwanja vya ndege na wananchi kwa jumla kughadhabishwa na mikataba hiyo.

Chama cha Wanasheria nchini Kenya kimekaribisha hatua hiyo ya rais, lakini wametoa wito kwa serikali hiyo kuweka wazi hasara zilizotokana na kubatilisha mikataba hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Rais wa LSK, Faith Odhiambo, alikaribisha hatua ya Rais ya kufutilia mbali mapendekezo ya Ubia kati ya Kampuni ya Adani Group na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya na KETRACO, akibainisha kuwa kusitishwa kwa kandarasi hizo ni kwa manufaa ya umma.

"Tunashukuru kutathmini upya kwa Rais na msimamo wa Serikali kuhusu mikataba hii, na tunatambua kuwa ni hatua nzuri kuelekea utawala unaozingatia katiba."

"Zaidi ya hayo, tunatoa wito kwa serikali kuweka hadharani gharama na hasara zote zilizopatikana na kuhakikisha kuwa hatua zinazofaa zinachukuliwa ili kupunguza hasara kwa nchi," ilisema taarifa hiyo.

Vile vile LSK ilisisitiza haja ya kuhakikisha uzingatiaji mkali wa katiba.

"Itakuwa kinyume na wajibu wa Serikali kuchukua hatua kwa manufaa ya umma ikiwa utambuzi wa kuchelewa wa masuala yanayohusu mikataba ya Adani ulikuja baada ya hayo hayo kutekelezwa," LSK ilisema.

Odhiambo pia aliitaka Serikali kuzingatia maoni ya Wakenya kuhusu masuala yanayowahusu.

"Tunawahimiza umma kwa usawa kusalia macho katika kulinda uhuru wa watu wa Kenya na kuzingatia maadili ya kitaifa na kanuni za Utawala chini ya Kifungu cha 10 cha Katiba," taarifa hiyo ilisema.

Haya yanajiri kuhu mamlaka moja nchini Marekani ikimshtaki mmiliki wa Kampuni ya Adani Holdings Limited ya India, bilionea Gautam Adani na watendaji wengine saba kwa tuhuma za rushwa na ulaghai wa dhamana kwa majukumu yao katika mpango wa mabilioni ya dola ili kupata fedha kutoka kwa wawekezaji wa Marekani na taasisi za kifedha duniani.

TRT Afrika