Rais William Ruto amefanya mkutano na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya mtandawo wa TikTok Shou Zi Chew/ Picha ya  Ikulu ya Kenya 

Serikali ya Kenya inasema itafanya kazi na huduma ya video ya TikTok katika kukagua na kufuatilia maudhui yake ili kuhakikisha kuwa inafuata miongozo na viwango vilivyokubaliwa vya jumuiya.

Rais William Ruto amefanya mkutano na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya mtandao wa TikTok Shou Zi Chew ambaye pia alikubali kuanzisha ofisi nchini Kenya ili kuratibu shughuli zake katika eneo hilo.

Hatua hiyo, Rais William Ruto alisema, itahakikisha kuwa maudhui kwenye jukwaa yanazingatia miongozo iliyokubaliwa.

Mkutano huu unafuata ombi lililofikishwa mbele ya spika wa bunge kwamba TikTok ipigwe marufuku Kenya kwa sababu inaharibu maadili ya jamii.

Kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya Kenya, Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok Shou Zi Chew, alijitolea kuhakikisha kuwa maudhui yanadhibitiwa ili kupatana na viwango vya jamii.

"Maendeleo haya mapya yanamaanisha kuwa maudhui yasiyofaa au yanayokera yataondolewa kwenye jukwaa," taarifa hiyo imesema.

Mapato kutoka kwa mitandao ya kijamii

Kenya pia imefikia makubaliano na majukwaa ya kimataifa ya kidijitali kuhusu uchumaji wa maudhui.

Rais William Ruto alisema Youtube, X.com (zamani Twitter) na Facebook zimekubali kushinikiza mapato kutoka kwa maudhui yaliyoundwa na vijana.

"Kuanzishwa kwa uchumi thabiti wa ubunifu ndio kipaumbele chetu," alisema.

Alibainisha kuwa Serikali imeshirikisha uongozi wa kampuni hizo kwa lengo la kuwapa Wakenya fursa za vipawa.

TRT Afrika