Serikali ya Kenya imefunga ubalozi wake katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, wakati mapigano kati ya makundi mawili yanayopigana yakiingia mwezi wa pili.
"Yani hili ni zoezi la kawaida kabisa, kwani Kenya lazima ilinde wananchi wake kwa njia yeyote ile kwani bunge na nchi litauliza maswali mengi juu ya hatua zilizochukuliwa kuhakikisha usalama wa ananchi wake wasipofanya hivyo." Aeleza mchambuzi wa siasa na mataalamu wa mambo ya nje kutoka Kenya, Dkt Edgar Githua.
Akiongeza kuwa jengo kurekebishwa ni rahisi lakini uhai wa mtu hauwezi kurudhishwa kamwe. " Kumbukeni kuwa mwaka 2012 kule Benghazi nchi ya Marekani ilishindwa kumtoa balozi wao wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya kana kwamba balozi akauawa." asema Dkt Githua.
Dkt Githua, wakati wa maongezi na TRT Afrika, akaongeza kuwa isiwe tabu maana mchakato wa kutafuta amani unawezekana hata nje ya nchi kwani haitabadilisha msimamo wa kidiplomasia wala harakati za Mamlaka ya Maendeleo ya Serikali Kuu, IGAD, kutafuta amani nchini Sudan.
Hatua ya ongozi wa Kenya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Alfred Mutua, ameiambia TRT Afrika kuwa ubalozi huo utafunguliwa tu baada ya hali kurudi katika hali ya kawaida Khartoum.
"Tutafungua ubalozi baada ya utulivu kurudi nchini," alisema Mutua.
"Tunatarajia kupata suluhisho nzuri kwa amani na maendeleo ya Sudan wakati wa Mkutano wa IGAD unaofanyika huko Djibouti tarehe 12 Juni. Sudan ni mwanachama wa IGAD," aliongeza.
IGAD, ambayo makao makuu yake makuu yapo Djibouti, ni chombo cha nchi ya wanachama nane. Nchi hizo ni Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Eritrea, na Uganda.
Lengo lake ni kusaidia juhudi za nchi wanachama katika amani, usalama, kilimo, mazingira, ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya kijamii.
Uamuzi wa Kenya wa kufunga ubalozi wake Khartoum unakuja kutokana na mashambulizi wakati mapigano yanaendelea kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF.
"Hata hivyo, ubalozi utaendelea kusaidia kuwahamisha raia wa Kenya," alisema Mutua.
Mapigano yalizuka Sudan tarehe 15 Aprili baada ya wiki kadhaa za mvutano kati ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), kikundi cha ulinzi wa ndani kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, na jeshi, kinachoongozwa na Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Wakuu hao wawili walikubaliana kulinda raia dhidi ya madhara, lakini mapigano yanaendelea kusababisha majeruhi, uharibifu na watu kuhama makazi yao Khartoum.
Kenya sasa inajiunga na Marekani, Kanada, Uswisi, Uholanzi, Japani, na Ufaransa katika kufunga ubalozi wake nchini Sudan.