Bunge ya Kenya imeanza uchunguzi kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa maadili unaofanywa na wanajeshi wa Uingereza nchini Kenya, maarufu kama BATUK.
BATUK ni kitengo cha mafunzo cha muda chenye makao yake makuu mjini Nanyuki, kilomita 200 kaskazini mwa Nairobi, lakini chenye kipengele kidogo jijini Nairobi.
Chini ya makubaliano na Serikali ya Kenya, Uingereza ina vikosi sita vya askari wa miguu kwa mwaka na hufanya mazoezi ya wiki nane nchini Kenya.
Kamati ya bunge ya ulinzi, kijasusi na uhusiano wa kigeni imewataka wananchi kuwasilisha nyenzo kwa ajili ya uchunguzi wa kitengo hiki cha wanajeshi kabla ya tarehe 6 Oktoba.
Kitengo hicho kimekuwepo nchini Kenya kwa miongo kadhaa katika kile ambacho Uingereza inaita "mshirika wetu wa ulinzi katika Afrika Mashariki."
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza haikujibu mara moja ombi la maoni Jumanne.
Uingereza ina takriban wanajeshi 200 wanaoishi nchini Kenya, wengi wao wakiwafundisha zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Kenya mwaka mmoja kabla ya kutumwa katika nchi jirani ya Somalia kupambana na kundi la waasi la al-Qaida la Afrika Mashariki, al-Shabaab.
Serikali ya Uingereza inawekeza zaidi ya $9.6 milioni kila mwaka katika ushirikiano huo.
Lakini baadhi ya Wakenya wameibua wasiwasi kuhusu jinsi majeshi ya Uingereza yanavyowatendea wenyeji pamoja na mazingira wakati wa mafunzo yao ya kijeshi.
Kenya inachunguza nini?
Taarifa kutoka kamati ya bunge ya ulinzi, kijasusi na uhusiano wa kigeni inasema uchunguzi utahusiha maswala haya:
- Kuchunguza tuhuma za ukiukaji wa maadili unaohusishwa na utovu wa maadili ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na tabia nyingine za kimaadili.
- Kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, mauaji au ukiukaji wowote wa viwango vya haki ya binadamu vinavyotambulika kimaadili.
- Kutathmini uadilifu wa operesheni ya BATUK hasa itifaki za usalama, kufuata mahitaji ya kisheria na kufuata viwango vya kijeshi vilivyowekwa.
Kutafuta haki
Mwishoni mwa 2021, polisi wa Kenya walisema wanafungua tena kesi ya mwanamke wa eneo hilo, Agnes Wanjiru, anayedaiwa kuuawa na mwanajeshi wa Uingereza mwaka wa 2012 na kupatikana kwenye tanki la maji ya taka.
Wabunge wa Kenya mwezi Aprili waliidhinisha mkataba mpya wa ushirikiano wa miaka mitano wa ulinzi na Uingereza na kupiga kura kupendekeza wanajeshi wa Uingereza wahukumiwe kwa mauaji.
Serikali ya Uingereza imesema imekuwa ikishirikiana kwa kesi ya Wanjiru.
Mwenyekiti wa kamati ya bunge, Nelson Koech, mapema mwaka huu alisema uchunguzi huo "utatoa fursa kwa Wakenya waliodhulumiwa kupata haki hatimaye, na kwamba hii itakuwa nguzo muhimu kwa azimio la kamati ya kuhakikisha Kenya inawajibisha wanajeshi wa kigeni, kukiuka sheria katika ardhi ya Kenya.”