Kenya bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu tangazo la Umoja wa Mataifa kuwa Marekani imesitisha ufadhili wake nchini Haiti.
Kuna takriban polisi 900 na wanajeshi kutoka Kenya, El Salvador, Jamaica, Guatemala na Belize katika mpango huo ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya dola milioni 13 za ufadhili wa Marekani kwa kikosi cha usalama cha kimataifa kinachosaidia kupambana na magenge yenye silaha nchini Haiti zimesitishwa chini ya siku 90 za Rais Donald Trump kusitisha msaada kwa mataifa ya kigeni, Umoja wa Mataifa ulisema.
Magenge yenye silaha zinazouzwa kwa kiasi kikubwa kutoka Marekani, yameungana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince chini ya muungano wa pamoja na sasa yanadhibiti sehemu kubwa ya jiji hilo na yanaenea katika maeneo ya karibu.
"Marekani ilikuwa imeahidi dola milioni 15, dola milioni 1.7 kati ya hizo zilikuwa tayari zimetumika, kwa hivyo dola milioni 13.3 sasa zimesitishwa," Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric aliwaambia waandishi wa habari.
"Tulipokea taarifa rasmi kutoka kwa Marekani ikiomba kusitisha shughuli mara moja kuhusu ufadhili wao."
Ujumbe wa kimataifa wa usalama wa Haiti unaoongozwa na Kenya , ingawa umeidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, sio operesheni ya Umoja wa Mataifa na kwa sasa inategemea michango ya hisani.
Kufikia sasa vikosi hivyo vimesaidia kwa kiasi fulani kurejesha hali ya utulivu.
Zaidi ya dola milioni 110 zimelipwa katika mfuko wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya operesheni hiyo, zaidi ya nusu yake ikiwa zinatoka Canada, kulingana na data za Umoja wa Mataifa.
Nini kitafanyika?
Marekani kwa jumla chini ya Rais Joe Biden ilikuwa imeahidi dola milioni 300 kwa ajili ya ujumbe huo.
Kwa vile mchango ni kwa hiari , nchi nyingi hazina ulazima wa kutoa fedha zozote kwa mpango huo.
Haijulikani kwa sasa ikiwa nchi kama Canada zitaongeza ufadhili wake kwa ujumbe huo kuziba pengo la ahadi ya Marekani.
Kwa sasa hakuna ushawishi wowote kwa Umoja wa Mataifa kuongeza ujumbe huo uwe chini ya ujumbe wa UN huku tayari ikiwa na changamoto ya mizozo mingine duniani.
Kenya bado haijatoa taarifa yoyote kuhusu uamuzi huu, na kama itaendelea kuwepo na maafisa wake wa polisi nchini Haiti au itawaondoa, kwani hakuna uhakika kama wana uwezo wa kuweka vikosi hivyo nchini Haiti kwa sasa.