Kenya imekana kuwa Marekani kusitisha kutoa fedha kwa ajili ya mpango wa amani nchini Haiti kutaathiri maafisa wake walio huko.
Ujumbe wa amani wa takriban maafisa 900 nchini Haiti, MSS unaongozwa na Kenya ambayo ina maafisa 617 wa polisi.
Lengo la Kenya ni kupeleka maafisa 1000 kwa jumla.
" Madai kwamba Marekani kusitisha ufadhili kwa ujumbe wa amani unaoongozwa na Kenya nchini Haiti, kutaathiri oparesheni hiyo, siyo kweli na hayana msingi wowote," Msemaji wa Serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema katika taarifa.
Mfuko wa Udhamini wa Umoja wa Mataifa kwa Haiti ulianzishwa Oktoba 2023.
" Ujumbe wa amani wa Haiti, MSS unaoongozwa na Kenya una vikosi vya polisi siyo kutoka Kenya tu bali Guatemala, Jamaica, El Salvador, Bahamas na Belize miongoni mwa mataifa mengine," Korir Sing'Oei, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Kenya ameeleza.
Amesema kufikia mwishoni mwa 2024, dola milioni 110.3 zilikuwa zimeahidiwa na nchi kadhaa zikiwemo Marekani, Canada, Ufaransa, Uhispania, Italia na Algeria.
" Dola milioni 85 zilikuwa zimepokewa na mfuko huo wa UN ikijumuisha kiasi kikubwa kutoka Marekani," Ameongeza.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa Marekani ilikuwa imeahidi kuchangia dola milioni 15 kwa mfuko huo, lakini imetoa dola milioni 1.5 na serikali ya Rais Donald Trump ikasitisha dola milioni 13.3.
" Ingawa mchango wa Marekani wa dola milioni 15 ambao haujalipwa kwa Mfuko wa UN umesitishwa kulingana na agizo la rais, Mfuko huo una fedha za kutosha kuendelea na mpango wa amani hadi mwisho wa Septemba 2025.
Katibu huyo mkuu amesema iwapo ujumbe huo utaidhinishwa na Umoja wa Mataifa kama kikosi cha UN kutahakikisha muendelezo wa ufadhili na kuufanya uwe miongoni mwa vipaumbele vyao vinavyotegemea na Kenya pamoja na washirika wote.