Kenya inalenga kuwaangamiza Kunguru milioni moja kutoka pwani ya nchini hiyo kabla ya mwisho wa mwaka 2024.
Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya (KWS), limetangaza utekelezaji wa mpango wa kuwaua kunguru hao kabla ya tarehe 31 Disemba 2024.
Mkurugenzi wa wanyamapori na huduma za Jamii Profesa Charles Musyoki, ameeleza kuwa mpango huo wa kuwaondoa kunguru wa nyumbani ni kwa ajili kulinda afya za watu dhidi ya ndege hao wakubwa weusi na kuongeza kuwa serikali itashughulikia tatizo hilo.
Ndege hao wametajwa kuwa kero haswa kwa wakazi na watumiaji wa huduma za hoteli katika maeneo ya pwani ya Mombasa, Malindi, Watamu na Kilifi.
Kunguru ni ndege wa kawaida wa familia ya kunguru (Corvidae) wajulikanao kama Kunguru wa nyumbani (Corvus splendens) wenye asili ya bara Asia.
Kwa sasa, viumbe hao wametapakaa maeneo mengi duniani tangu walipofika kwenye ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki kwa njia ya meli.
Nchini Kenya, ndege hao walianza kuingia kwenye miaka ya 1947 huku idadi yao ikizidi kuongezeka tangu wakati huo na kuwa changamoto maeneo ya pwani, wakati kwa upande wa Tanzania, ndege hao maarufu kama Kunguru wa Zanzibar, waliingia nchini humo kutoka India kusaidia kuokota taka maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, viumbe hao wamegeuka kuwa kero kwa jamii, hasa kutokana na kuchafua mazingira na kuharibu miundombinu ya umeme.